Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliotimuliwa Nunge walala kwa mafungu

19499 Pic+waliotimuliwa TanzaniaWeb

Thu, 27 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni mwezi mmoja umepita sasa tangu Serikali ilipowataka vijana waliokuwa wakiishi katika Kambi ya Wazee ya Nunge iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam kuondoka kambini hapo.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, mkuu wa wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri aliwataka vijana 34 waliokuwa wakiishi kwenye kambi hiyo kuondoka kwa hiyari kabla Serikali haijatumia nguvu kuwaondoa eneo hilo.

Nililazimika kurudi kambini hapo kutazama utekelezaji wa agizo la Serikali la kuwafungashia virago vijana hao ndipo nilipokutana na vilio vya namna mbalimbali vilivyotokana na uamuzi huo.

Alala nje tangu atimuliwe

Nikiwa kambini hapo nikakutana na mmoja wa vijana waliokuwa kwenye kundi la waliotakiwa kuondoka na kupewa saa 24 kuondoka kwa hiyari kabla Serikali haijatumia nguvu kuwaondoa.

“Nitakwenda wapi sina ndugu, ni mgonjwa miguu yangu yote miwili nimewekewa vyuma baada ya kupata ajali,” alisema kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Adamu Msafiri.

Anasema tangu Septemba 2, mwaka huu alipotolewa vyombo vyake na kutakiwa aondoke amekuwa akilala nje kambini hapo. “Sina ndugu yeyote hapa Dar es Salaam jua, giza na baridi vyote vinaniishia mwilini”.

Msafiri anasema agizo la Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kuhusu kuondolewa kwa vijana hao lilitolewa Januari 4, mwaka 2016 lengo likiwa ni kutaka kuona kambi inasalia kuwa ya wazee kama ilivyo kwenye malengo ya kuanzishwa kwake.

Akisimulia namna alivyofika kambini hapo, Adamu anasema alipelekwa mwaka 2012 na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wakati huo (hamkumbuki jina) baada ya kuonekana hana ndugu jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Anasema yeye ni mwenyeji wa Liwale mkoani Lindi na alikuja Dar es Salaam mwaka 2011 ambapo kwa bahati mbaya alipata ajali ya gari ambayo ilisababisha miguu yote kuvunjika na kulazwa katika hospitali hiyo.

“Nililazwa Muhimbili ambapo nilifanyiwa upasuaji na kuwekewa vyuma kwenye miguu yote miwili, hivyo kutokana na matibabu yangu kuwa ya muda mrefu nilitakiwa nisikae mbali na hospitali,” anasema Adamu.

Adamu anasema miezi tisa ilipopita alifanyiwa upasuaji mwingine na baada ya wiki mbili aliruhusiwa na kutakiwa kila baada ya wiki mbili arudi hospitalini hapo.

Kwa kuwa alikuwa hana ndugu jijini Dar es Salaam ndipo katibu mkuu huyo alipomchukua na kumpeleka Kambi za Wazee ya Nunge ili aweze kuishi hapo.

Anasema Lengo kubwa la kukaa kwenye nyumba hizo ni kutaka urahisi wa kwenda Muhimbili tofauti na endapo angerudi Liwale ambako asingeweza kuwahi matibabu kwa wakati.

“Kutokana na hali hiyo ndipo Serikali ilipoamua kunileta hapa mwaka 2012. Niliweza kuendelea na matibabu kila nilipohitajika hospitalini,” anasema.

Hata hivyo, anasema kutokana na ugumu wa maisha wakati mwingi alikuwa akikosa nauli ya kwenda hospitali hivyo kumfanya aishi katika mazingira magumu.

Anasema kutokana na hali hiyo, alitafutiwa fundi aliyemfundisha ufundi wa luninga, pasi, feni na blenda ya kusaga matunda ili baadaye atakapokuwa amewiva na kumudu vyema ufundi huo, utamsaidia kujipatia kipato cha kuendeshea maisha yake.

“Namshukuru Mungu wateja walikuwa wanakuja hapa kambini ili niwatengenezee vifaa vyao nami niliweza kupata fedha ya nauli na nyingine ilinisaidia kwenye matibabu,” anasema Adamu.

Anasema kilichomshangaza ni wakati wa kutekeleza agizo la Serikali alipotolewa nje vitu vyake na kuharibiwa kwa vifaa vya ufundi pamoja na vitu mbalimbali vya wateja zikiwemo luninga na pasi zilizoletwa kwa ajili ya matengenezo ambapo sasa anadaiwa.

“Waziri mwenye dhamana naomba nisikilize kilio changu, nisaidie ili niweze kuruhusiwa kurudi kwenye nyumba hizi sina ndugu na ninatakiwa nifanyiwe upasuaji mwingine wa miguu yote miwili sina pa kwenda nitaendelea kulala hapa hapa nje,” anasema.

Wanne chumba kimoja

Naye Abdallah Issa ambaye pia ni miongoni mwa vijana walioondolewa kwenye kambi hiyo, anasema baada ya kutimuliwa Nunge, wamekuwa na wakati mgumu kimaisha hususani katika malazi.

Anasema baada ya kutimuliwa aliungana na wenzake wanne ambapo walitafuta chumba cha giza wanacholipia kodi ya Sh25,000 kwa mwezi ambapo sasa wote wanalala humo (mchongoma).

Issa anasema kwa kuwa walitakiwa kulipa fedha ya miezi sita kila mmoja alitoa Sh37,500 na kwamba fedha hizo ni sehemu ya Sh100,000 walizopewa na Serikali kwa ajili ya kujikimu kimaisha.

Hata hivyo, anasema fedha walizopewa hazikuweza kutosheleza mahitaji kwa kuwa zilitumika kuhamishia mizigo, kupanga chumba na bado wanahitaji matumizi mbalimbali ya lazima ikiwemo chakula.

“Kabla ya kuondolewa kambini kila mmoja tulipewa Sh100,000 kwa ajili ya kujikimu kimaisha. Si unajua hiyo hiyo upange chumba na ufanye matumizi mengine, je kitabaki kitu gani? Kwetu maisha ni magumu mno,” anasema Issa.

Anayeishi ukweni asimulia

Naye Nicholaus Kasato (23) anasema alichofanya ameamua kwenda kuishi kwenye nyumba ya wazazi wa mke wake (ukweni) huku akiendelea kujipanga kimaisha ili kutengeneza mikakati ya kupanga chumba chake hapo baadaye.

Anasema wazazi wake walifariki akiwa na miaka miwili na kwamba wote walikuwa wakiishi katika kambi hiyo ya wazee ambapo baadaye uongozi wa kambi ulimhamisha na kumpeleka kwenye Makazi ya Makao Makuu ya Taifa ya Watoto Kurasini.

“Namshukuru Mungu nilisomeshwa kuanzia awali hadi kidato cha nne, lakini mwaka 2016 nilihamishwa tena na kurudishwa Nunge. Nikiwa hapa nilimpata mfadhili ambaye alinisomesha udereva katika Chuo cha Ufundi Veta, lakini sijabahatika kupata kazi, hivyo nikipata kibarua chochote kwa sasa nipo tayari kukitekeleza ili kunusuru maisha yangu,” anasema Kasato.

Ustawi wa Jamii wafafanua

Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto, Rabikira Mushi anasema kila kijana alilipwa Sh100,000 ambazo waliahidiwa na Serikali kwa ajili ya kujikimu kimaisha.

Anasema kati ya vijana hao 20 walijiunga na mafunzo ya Jeshi la Akiba (mgambo) ambapo Serikali iliwagharamia gharama zote za mafunzo ambayo yalianza Septemba 3, mwaka huu na kutarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu.

Kamishna Mushi anasema vijana hao walipelekwa kwenye kambi hiyo mwaka 2016 wakitokea Makao Makuu ya Taifa ya Watoto Kurasini na kwamba walikuwa wakipatiwa huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo elimu ya msingi hadi sekondari na wengine walikwenda vyuo vya ufundi na hata vyuo vikuu.

“Kilichojitokeza kwa vijana hao hawakuweza kujiimarisha kwenye nyanja mbalimbali walizopelekwa kwa ajili ya kujiandaa kujitegemea matokeo yake umri wao ukawa mkubwa hivyo tukalazimika kuwatoa kwenye makazi ya watoto Kurasini na kuwahamishia kambi hii ya wazee.

“Vijana hao wana umri kati ya miaka 23 hadi 40 mazingira hayaruhusu kuishi kambini hapa, hivyo tunataka waende wakajichanganye uraiani kwa kuwa maisha yao yote hawakuwahi kujichanganya na watu wengine,” anasema Mushi.

Jinsi ya kuasili Mtoto

Akieleza jinsi ya kuasili mtoto aliyefiwa na wazazi wote na hana ndugu, alisema kuna utaratibu umewekwa ambapo Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2009 imefafanua kila kitu.

Anasema kama kuna mtu mwenye miaka kuanzia 21 hadi 50 anayemtaka mtoto yatima anaweza kuasili ambapo wakati akiendelea kuishi na mtoto huyo atapewa miezi mitatu ya kwanza na baadaye watamuongezea mitatu mingine.

Lengo la kufanya hivyo ni ili maofisa wa ustawi wa jamii kuweza kumfuatilia aliyeomba kuishi na mtoto na watamtazama tabia na ukaribu alionao kwa mtoto huyo.

Baadaye maofisa hao watawafuatilia ndugu wa karibu, majirani ili kupata kauli zao kwa jinsi wanavyomjua ndugu yao kitabia na endapo watajiridhisha kwamba mhusika hana tatizo huruhusu kuasiliwa kwa mtoto ambapo kuanzia hapo atapata haki zote za msingi anazostahili.

Chanzo: mwananchi.co.tz