Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliosamehewa na JPM Arusha waondolewa nafasi zao

SHANAA Waliosamehewa na JPM Arusha waondolewa nafasi zao

Thu, 25 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KAMANDA wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana na Mkuu wa TAKUKURU mkoani humo, Frida Wikes, ambao Rais John Magufuli alitangaza kuwasamehe, wameondolewa kwenye nafasi hizo.

Jumatatu, Rais Magufuli wakati akiwaapisha viongozi aliowateua Ikulu jijini Dar es Salaam, alitangaza kuwasamehe viongozi hao ambao walikuwa wakifanya kazi ambazo hajawatuma.

Taarifa za kuondolewa kwao zilisambaa jana kwenye mitandao ya kijamii ambapo Nipashe ilizithibitisha kupitia mamlaka wanazozifanyia kazi ambazo zilikiri ni za kweli.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, (IGP), Simon Sirro, aliliambia gazeti hili kuwa, ni kweli Jeshi la Polisi limemuondoa Kamanda Shana na kumwamishia Chuo cha Polisi Moshi, mkoani Kilimanjaro.

“Ni kweli ameondolewa, hayo ni mabadiliko ya kawaida ndani ya Jeshi la Polisi, tuliona kuna upungufu pale chuoni tukampeleka kuongeza nguvu, ameondolewa leo (jana),” alisema.

Naye, Ofisa Uhusiano wa TAKUKURU, Doreen Kapwani, alikiri taasisi hiyo imemuondoa Wikes na kumwamishia Makao Makuu.

Akizungumza siku hiyo, Rais Magufuli alisema: “Leo nilikuwa niwatoe RPC (Kamanda wa Polisi) pamoja na Mkuu wa TAKUKURU, Arusha nimeona niwaonye hapa hapa, nimeamua kuwasamehe, lakini sijawasamehe moja kwa moja wakifanya kosa lolote wataondoka.

“Ninataka wakafanye kazi nilizowatuma siyo kazi wanazojituma wao, ninajua mtawafikishia salamu nimejitahidi sana kuwasamehe.”

Alisema haiwezekani ukawa umewatuma watu wakafanye kazi za serikali wanafanya shughuli zao.

“Nyinyi mnafahamu shughuli walizokuwa wanazifanya hasa katika kipindi hiki kifupi, Mkuu wa Mkoa kawafikishie ujumbe.

“Wafanye kazi walizotumwa kulingana na mamlaka yao wasimamie sheria, maadili yao na kwa Arusha,” Rais Magufuli alisema siku hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live