Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliooa mitala wadaiwa kutelekeza wake, watoto Ngorongoro

Mitala Ngorongoro B69b30ecbd9e 780x470 Waliooa mitala wadaiwa kutelekeza wake, watoto Ngorongoro

Mon, 17 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WANAWAKE walioolewa zaidi ya mmoja katika boma la kimaasai, wanaoishi Kijiji cha Kayapus Kata ya Ngorongoro, wameiomba serikali kuwasaidia, ili nao waweze kuishi na watoto wao kwa madai baadhi ya waume zao hawakuwaandikisha katika mchakato wa kuhama.

Wamedai hawakatai kwenda kuishi Msomera, wilayani Handeni, lakini baadhi ya waume zao hawajawashirikisha katika mchakato wa kuondoka kwao, badala yake wameshirikisha mke au wake wanaowapenda na kuandika majina yao na kuwaacha wake wenza wengine wakihangaika na watoto.

Wakizungumza katika kijiji hicho, wakiongozwa na Namuruu Pariti na Ndetia Mollel wamedai wao ni wake wenza, lakini waume zao walishirikisha baadhi ya wake wanaowapenda na kuwaacha wengine na watoto.

“Mimi sina nyumba, nataka nami nipewe nyumba yangu mwenyewe, lakini siwezi kukaa na mke mwenzangu nyumba moja, naomba serikali inipe nyumba, maana nami ni mke na nina watoto wa mume huyo huyo mmoja,” amedai Namuruu.

Amedai baadhi ya wanaume hawajali familia zao na kusababisha watoto wasipate chakula kama haki zao za msingi, hali inayosababisha wake zao kuomba kwa majirani.

Akizungumzia hilo Pariti Kondoro, ambaye yeye ni miongoni mwa wanaume wenye wake zaidi ya mmoja, alikiri ni kweli baadhi ya wanaume wameandikisha wake wanaowapenda na kuacha kuandikisha wengine, hali inayoibua migogoro ya kifamilia na kusababisha watoto na mke au wake kukosa chakula.

Ameiomba serikali kuangalia kwa ukaribu suala hilo, ambalo wake wenza wameolewa ndani ya boma moja, ili nao waweze kupata makazi yao wanapohamia Msomera wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live