Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliokwama Lindi watia shaka saa 72 za Bashungwa, yeye asisitiza lazima iishe

Daraja La Lindiiii Waliokwama Lindi watia shaka saa 72 za Bashungwa, yeye asisitiza lazima iishe

Wed, 8 May 2024 Chanzo: Mwananchi

Wakati saa 72 zilizotolewa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kwa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) kukamilisha ujenzi huo zikikamilika, uwezekano kazi hiyo kukamilika ndani ya muda huo uko mbali kutokana na wingi wa maji eneo hilo.

Mwananchi limeweka kambi katika Kijiji cha Matandu na kujionea shughuli ya ujenzi wa daraja la muda mfupi la Matandu ambalo ni moja kati ya madaraja mengine manne yaliyokatika mkoani Lindi na kukatisha mawasiliano.

Juzi na jana Waziri Bashungwa alitembelea ujenzi wa barabara na madaraja yaliyokatika na kujionea shughuli hiyo inavyokwenda huku akisisitiza kwamba kazi hiyo inatakiwa kukamilika ndani ya saa 72.

Mbali na Matandu, sehemu nyingine iliyoharibiwa ni Somanga ambako daraja limesombwa na maji na kusababisha ugumu wa mawasiliano kati ya wasafiri wanaotoka Dar es Salaam kwenda kusini ya Lindi na Mtwara, na kinyume chake.

Mwananchi imezungumza na baadhi ya madereva jana Mei 7, 2024 wakieleza kuwa hakuna uwezekano wa kazi hiyo kukamilika ndani ya saa 72 kwa kuwa maji bado ni mengi yanatiririka hasa huko Matandu.

“Natokea Mtwara kufuata saruji, naelekea Dar es Saalam, hapa tunavyoona ujenzi unavyokwenda, hawatamaliza kesho. Sikatai maji leo yamepungua kwa kiasi kikubwa lakini hapa kwenye daraja maji ni mengi, kiukweli hizi saa 72 alizosema Waziri si kweli, haitakamilika. Ningemwomba Waziri awaongeze muda kuliko kusema saa 72 likamilike,” amesema Said Abdallah.

Dereva mwingine anayetoka Mtwara kwenda Dar es Salaam, Salum Haji amesema matumaini ya kumalizika kwa daraja hilo ndani ya saa 72 hayapo, amewaomba viongozi wote wa Serikali akiwemo Waziri wa Ujenzi, waliangalie jambo hili.

“Mimi sio mkandarasi wala mtaalamu wa ujenzi lakini kwa macho ya kawaida, hawawezi kumaliza kwa saa 72, hapa kwenye daraja, maji bado ni mengi, kujaza mawe leo kesho wamalizie sio kweli,” amesema Haji.

Wananchi wafungua

Abiria aliyekuwa akisafiri kwa lori kutoka Mtwara kwenda Pwani, Maimuna Juma ameiomba Serikali iangalie namna ya kufanya, waongezewe muda ili wakandarasi waweze kujenga kwa ufanisi zaidi.

“Japo tumekaa sana leo siku ya nne tuko hapa, lakini kwa maagizo aliyoyatoa Waziri kwa saa 72 ili daraja likamilike, sio kweli,” amesema Maimuna.

Kutokana na kukosa huduma mbalimbali za kijamii baadhi ya malori yameondoka katika eneo la Matandu na kwenda kuegesha kwenye hoteli.

Mmoja wa madereva hao, Abdallah Selemani amesema kutokana na mazingira ya eneo la Matandu, kuwa siyo rafiki wenzao wameamua kuondoka na kwenda kupaki kwenye mahoteli kwa kuwa hakuna uhakika wa kuondoka Alhamisi.

Upatikanaji wa huduma za jamii katika eneo la Matandu umekuwa hatarishi kwa kuwa hakuna vyoo wala maji ya kuwasaidia, hali inayoweza kusababisha magonjwa ya mlipuko.

Mariamu Alex amesema inawalazimu kwenda kujisitiri kwenye vichaka japo wanahofia kukutana na wadudu wabaya lakini hawana namna nyingine.

Upatikanaji wa chakula

Hali ya upatikanaji wa chakula katika eneo la Matandu ni changamoto kwani wenyeji wanaoishi katika eneo hilo wamekuwa wakiuza chakula kwa bei juu, sahani moja ya wali au ugali ikiuzwa Sh5,000.

Baadhi ya wasafiri waliokwama wameshindwa kumudu gharama hizo, hivyo wameamua kula mlo mmoja kwa siku yaani usiku tu.

“Tunaomba Serikali itusaidie chakula, sisi wengine hatuwezi kumudu gharama za maisha, hasa chakula. Ndio maana mimi kwa siku nakula usiku tu, na wakati mwingine nakula maandazi tu,” alisema.

Bashungwa asisitiza lazima iishe

Hata hivyo, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema hatasita kubadilisha timu ya wataalamu na mkandarasi wanaoendelea na kazi ya kurejesha mawasiliano ya barabara hiyo kutokana na kasi ndogo ya kazi na usimamizi.

Bashungwa amesema hayo leo Mei 7, 2024 baada ya kutoridhishwa na usimamizi na kasi ya urejeshaji wa mawasiliano katika eneo hilo na kumtaka mkandarasi kuongeza kasi ili wamalize zoezi ndani ya muda uliotolewa.

"Mimi naweza kufukuza timu yote, bora niwaambie Watanzania timu hii imefeli na niagize nyingine ambayo inaweza ikaja kufanya kazi, hatuwezi kwenda hivi," amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amemwagiza Mkurugenzi wa Matengenezo ya Barabara wa Tanroads kutafuta na kuongeza magari ya kubeba mawe na vifusi pamoja na mitambo ili kazi ifanyilke usiku na mchana bila kusimama.

Chanzo: Mwananchi