Wananchi wa Kata ya Uyole waliokubwa na mafuriko Januari 7 mwaka huu, wameiomba Serikali kuwapatia mikopo ili kuwawezesha kuanzisha miradi kutokana na maisha magumu wanayopitia.
Ombi hili wamelitoa mbele ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, baada ya kukagua miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika baadhi ya shule jijini hapa zilizopokea fedha kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania ( TEA) hususan kuchangia mifuko 100 katika Shule ya Sekondari Nsalaga.
Mhanga wa mafuriko, Yohana Mwaisela amesema kuwa tangu wakumbwe na janga hilo wamekuwa wakiishi maisha ya tabu ikiwepo mahitaji kama vyakula, kupeleka watoto shule kutokana na ukosefu wa kipato.
“Baadhi yetu tulikuwa wajasiriamali lakini baada ya mafuriko fedha na bidhaa mbalimbali zilisombwa na maji tunakuomba Spika na Mbunge Dk Tulia Ackson kupitia Taasisi yako Tulia Trust na Serikali tusaidiwe mikopo,” amesema.
Amesema licha ya kuwepo kwa hali ngumu ya maisha wanaishukuru Serikali kwa kuwasaidia baada ya kukumbwa na mafuriko kwa kuwapeleka magodoro, blanketi na mahitaji mengine ikiwa ni juhudi za mbunge ambaye amekuwa bega kwa bega na wananchi wake.
“Tunatambua juhudi na jitihada zako kwetu wananchi wanyonge na ujio wako leo utatufuta machozi kwani tangu tukumbwe na hadha ya mafuriko hatuna mitaji ya kutuwezesha kuishi. Tunaomba wewe binafsi na Serikali sikivu mtusaidie kupata mikopo,” amesema.
Naye Hanifa Joel aliyekuwa mfanyabishara wa mahitaji ya nyumbani, amesema anaomba mbunge wao kubeba ombi la mikopo na kulifanyia kazi kwa kutambua kuwa yeye ni mama wa wanyonge ambaye amekuwa mstari wa mbele kuona wanambeya wanafanya shughuli mbalimbali za kiuchumi.
“Tunajivujia uwepo wa Mbunge Dk Tulia Ackson kutokana na msaada mkubwa kwetu waathirika wa mafuriko kwani baada ya kutokea ulifika kutufariji na kuharakisha upatikanaji wa vifaa vya kujisitiri ingawa kwa sasa changamoto ni namna ya kuendesha maisha yetu ya kila siku,”amesema.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuwashika mkono wananchi wake na kwamba suala la mikopo amelichukua na kulifanyia kazi.
“Ndugu zangu Serikali yenu ni sikivu inasikiliza kilio chenu wananchi na niseme tu nimesikia na tunakwenda kulifanyia kazi pia niwatake kuwa kipaumbele kuchangia shughuli za mradi ya elimu ili kuunga mkono Serikali yenu,” amesema.
Kwa upande wake, Diwani Kata ya Nsalaga, Daniel Njango amesema kuwa utendaji wa kazi wa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, Mungu ndiye atamlipa kwa kuwa amewafuta machozi wana Mbeya baada ya kutokea janga la mafuriko katika kata hiyo.
“Tunakuona kwenye raha, shida za wanambeya sisi binafsi tunajivunia kuwa na kiongozi kiongozi wa Bunge licha ya kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini tunakupa ahadi uchaguzi Mkuu 2025 jua letu mvua yetu mpaka tone la mwisho tutakuwa sote,” amesema.