Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliokufa kwa mvua kubwa Dar wafikia 12

53f313f9f684fccfbe875656fb3d3c6c Waliokufa kwa mvua kubwa Dar wafikia 12

Fri, 16 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imesema kwamba watu 12 katika Jiji la Dar es Salaam, wamekufa baada ya kusombwa na mafuriko kutokana na mvua zilizoanza kunyesha Oktoba 13, mwaka huu na kuendelea hadi jana.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliyasema hayo jana wakati alipokutana na waandishi wa habari ofisini kwake kutoa taarifa ya hali ya mvua na athari zake ndani ya Jiji la Dar es Saalaam.

Kamanda Mambosasa alisema Wilaya ya Ilala ndiyo iliyoathiriwa zaidi kutokana na kupoteza watu wanane huku Kinondoni ikipoteza watu wanne na Temeke, Ubungo na Kigamboni zikiwa hazijaripoti kifo chochote.

Aliwataja waliofariki wilayani Ilala kuwa ni Mariam Yahaya (45) ambaye ni mkazi wa Vingunguti ambaye alisombwa na maji alipokuwa akijaribu kuokoa vyombo vyake vilivyokuwa vikisombwa na maji.

Mwili wake ulikutwa ukielea kando ya Mto Msimbazi na umehifadhiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Kwa mujibu wa Mambosasa, miili ya watu wengine watano ilipatikana katika bonde la Mto Msimbazi, eneo la Jangwani ambako wawili kati yao walifahamika kwa majina.

“Mwili wa kwanza ulitambulika kuwa ni Herieth Kanuti (18) ambaye ni mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika Shule ya Sekondari Rutihinda.

Mwingine ni wa Ipyana Mwakifuna (19) ambaye ni mkazi wa Jangwani ambaye ni askari wa Jshi la Akiba la Mgambo,” alisema Kamanda Mambosasa na kuongeza kuwa miili ya watu watatu haijatambuliwa ambayo ni ya wanaume wawili na mwanamke mmoja.

Aidha, alisema tukio lingine liliripotiwa Tabata, Oktoba 14, mwaka huu saa 12.45 asubuhi ambako mwili wa Philipo Feliciani (30) mkazi wa Tabata Kimanga ulionekana ukiwa umenasa katika matope katika Mto Tenge.

Alisema mwili mwingine wa mwanamume ambaye hajafahamika na ambaye anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 hadi 35 ulikutwa Mji Mpya, Ukonga. Kwa upande wa Kinondoni, alisema watu wanne walipoteza maisha wakiwamo watoto wawili wa familia moja na watu wazima wawili.

Aliwataja marehemu hao kuwa ni Ibrahimu Hassani (24) ambaye ni mkazi wa Kigogo Mbuyuni, Husein Awadhi (5) mkazi wa Kigogo Mbuyuni na Bakari Awadhi (14) ambaye pia ni mkazi wa Kigogo Mbuyuni.

“Watoto hao walisombwa na maji baada ya nyumba yao iliyopo katika eneo la Kigogo kujaa maji na watoto hao kushindwa kujiokoa. Huyo Ibrahim Hassani alikuwa akijaribu kumuokoa mtoto, lakini alishindwa naye kusombwa na maji,” alieleza Kamanda Mambosasa.

Alisema mwili mwingine wa mwanamume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 hadi 35 ulionekana ukielea Mabibo katika mfereji unaopeleka maji Mto Msimbazi na miili ya marehemu wote imehifadhiwa Muhimbili.

Mbali na vifo hivyo vilivyotokana na mafuriko, Kamanda Mambosasa alisema watu wengine watano wa familia moja walifariki dunia kwa ajali ya moto uliounguza nyumba Pugu Stesheni wilayani Ilala.

Alisema katika tukio hilo lililotokea saa nne kamili usiku wa Oktoba 13, mwaka huu, nyumba ya Edward Katema yenye vyumba vinne iliteketea kwa moto uliosababishwa na hitilafu ya umeme iliyoanzia katika swichi kubwa.

Aliwataja waliokufa kuwa ni Jackline Frank (27) na Edward Katemi (11) ambao ni wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Pugu na Esther Katemi (15) ambaye ni mwanafunzi katika Shule ya Msingi Pugu; Edson Katemi (10) mwanafunzi katika Shule ya Msingi Green Hill na Ivon Edward (4) ambao wote miili yao imehifadhiwa Muhimbili.

Katika hatua nyingine Kamanda Mambosasa alisema kampeni za Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli zimemalizika salama katika jiji hilo na kuwapongeza wananchi wake kwa kudumisha amani na utulivu.

Chanzo: habarileo.co.tz