Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliokimbia ARV kusakwa majumbani

10074 Arv+pic TZW

Tue, 26 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kahama. Siku chache baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuzindua kampeni ya kupima virusi vya Ukimwi, shirika lisilo la Serikali la Shdepha+ limeanza kuwabaini waathirika waliokimbia kuendelea na umezaji dawa za kufubaza makali ya ugonjwa huo ili kuwarejesha upya kwenye matumizi.

Kampeni hiyo ya Tulonge afya ilizinduliwa juzi ikilenga kuleta mabadiliko kwenye suala la matumizi ya dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi.

Akizungumza wakati wa kuitambulisha kampeni hiyo, meneja mkuu wa mradi wa afya ya Tulonge wilayani Kahama, Projestus Mwemezi alisema wameamua kuanzisha kampeni hiyo baada ya kubaini watumiaji dawa wamepungua huku maambukizi ya ugonjwa huo yakiongezeka kwa asilimia 7.3.

“Kauli zisizostahili zimekuwa chanzo cha waathirika hao kusitisha utumiaji dawa hizo hali inayosababisha kuongezeka kwa vifo, huku wengine wakilazimika kuhama vituo kuepuka kudhalilishwa,” alisema Mwemezi.

Alisema kampeni hiyo itahakikisha inawasaka watu hao wakiwamo vijana, kukaa nao na kuwaelimisha ili waendelee kutumia dawa hizo.

Mwemezi alisema utafiti uliofanywa na shirika hilo hivi karibuni umebaini kuwapo kwa mwitikio mdogo kwa wanaume katika suala la kupima afya zao na kwamba, kupitia kampeni hiyo watahamasisha vijana kuanzia miaka 10 hadi 30 kujitokeza kupima afya sambamba na kupatiwa elimu ya kujikinga.

Naye mkurugenzi wa mradi huo tawi la Kahama, Venance Mzuka alisema mradi utadumu kwa miaka mitano, utajikita katika kuleta mabadiliko makubwa ili jamii ione umuhimu wa kupata huduma kwa kuchunguza afya zao mapema kuliko kusubiri tiba baada ya kuugua.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kahama, Anderson Msumba alisema mradi huo utaleta mabadiliko chanya hasa kwa mtoto wa kike ambaye anaanza kujitambua.

“Ni vyema mtoto wa kike akajengewa uwezo wa kufahamu umuhimu wa afya ya uzazi ili amudu kujistiri na kutambua kuwa kinga ni bora kuliko tiba,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz