Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliokamatwa maandamano ya kwenda Ikulu wafikia 10

Waliokamatwa Maandamano Waliokamatwa maandamano ya kwenda Ikulu wafikia 10

Mon, 19 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu kumi na moja wanadaiwa kukamatwa na Jeshi la Polisi katika maandamano ya kupinga uwekezaji wa bandari yaliyokuwa yamepangwa kufanyika leo Jumatatu Juni 19, 2023 akiwemo mratibu wa wa wake, Deusdedith Soka.

Juni 15, 2023 Deusdedith Soka ambaye aligombea udiwani Chadema, Uchaguzi Mkuu wa 2020, alitangaza kuitisha maandamano kupinga mkataba wa ushirikiano wa uendeshaji wa bandari kati ya Kampuni ya DP World na Tanzania.

Hata hivyo Juni 17 Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lilipiga marufuku maandamano hayo na kueleza kuwa, mtu aliyeandaa maandamano hayo ameshajibiwa kwa barua akielezwa ni marufuku kufanyika maandamano yoyote.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Wakili Dikson Matata amesema ametoka kituo Kikuu cha Polisi ambapo watu kumi na moja wamekamatwa.

"Nimeongea na RCO amesema hawana nia mbaya nao na hivyo wakimaliza kuwahoji hakutakuwa na sababu nyingine ya kuendelea kuwa nao," amesema Wakili Matata.

Amewataja waliokamatwa ni pamoja na mratibu wa maandamano hayo

Deusdedith Soka, Remina Peter, Joel Msuya, Jacob Mlay, Fatma Thabit na Juma Kaswahili.

Wengine ni Elyneema Yuda, Rehema Zonga, Frank Erasto, Seleman, Mohamed Nikupe na Haji Baragomba.

Jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam. Jumanne Muliro zinaendelea baada ya kupokea simu na kuahidi kumtafuta mwandishi baadaye, alipotafutwa tena simu yake iliita bila kupokewa.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amekitahadharisha kikundi cha watu wanaopanga kufanya maandamano kupinga mkataba wa ushirikiano wa uendeshaji Bandari kati ya Tanzania na Kampuni ya DP World ya Dubai.

Pia amekemea upotoshwaji unaofanywa na watu wanaosema nchi imeuzwa na kwamba hata siku moja Rais Samia Suluhu Hassan hawezi kuuza nchi kwa kuwa ameapa kulinda nchi na kuwaletea maendeleo wananchi wake

Tahadhari hiyo imeitoa wakati akiongea na vyombo vya Habari ofisini kwake ikiwa ni muda mfupi baada ya Jeshi la Polisi kudhibiti maandamano yaliyopangwa kufanyika kwenda Ikulu kushinikiza kupinga mkataba huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: