Dar es Salaam. Baadhi ya wanawake wameanza kuondoka katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya kubaini taarifa kuwa leo Jumamosi Agosti 31, 2019 katika eneo hilo inatolewa mikopo kwa familia masikini na wajane si za kweli.
Mamia ya wananchi kutoka sehemu mbalimbali wamekusanyika katika uwanja huo linapofanyika tamasha la Ndoa na Familia ambalo mgeni rasmi ni mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Baadhi ya watu hao wamedai kupewa taarifa katika maeneo wanayotoka kuwa katika uwanja huo kuna taasisi kutoka nchini Korea inatoa mikopo kwa familia masikini na wajane, jambo ambalo si kweli.
Mwajuma Ramadhan amesema kinachoendelea ni tofauti na matarajio ya wengi waliopo uwanjani hapo.
“Sisi tumeambiwa leo tunakuja kuwaona hao wadhamini wetu ambao watatupatia pesa za kujikwamua kiuchumi lakini badala yake huko ndani kuna tamasha la amani na ndoa katika familia.”
“Tangu nimefika hapa kile tulichoahidiwa hakijagusiwa bora niondoke kama pesa zitatoka nitapata,” amesema Mwajuma.
Habari zinazohusiana na hii
Zainab Mussa, mkazi wa Makumbusho aliyeongozana na kikundi cha wanawake 43 amesema leo wamefika uwanjani hapo kuwaona viongozi, kubainisha kuwa fedha zitatolewa baadaye.
“Si mkopo ni ufadhili hivyo baadaye pesa hizo zitatolewa na kila mtu atajua nini azifanyie kwa sababu ni kwa ajili ya kaya maskini,” amesema Zainab.
Mkazi wa Kinyerezi, Mariam Isike amesema ili kupata fedha hizo walikuwa wakiandikisha majina katika ofisa ya mtendaji wa kata wakiambatanisha fomu iliyokuwa na taarifa zao kwa ufupi pamoja na picha ndogo.
“Na wakati tunakuja huku tulichanga Sh1,500 ya usafiri na hapa nilipo nimepotezana na wenzangu,” amesema.