Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliohitimu kidato cha nne 2018 wapewa fursa nyingine

Fri, 29 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Serikali imetoa nafasi kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2018 kufanya machaguo upya kuhusu tahasusi ‘combination’ wanazotaka kusoma.

Waziri wa nchi ofisi ya Rais-Tamisemi, Seleman Jafo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma amesema mfumo huo ni mpya lakini unalenga kuwasaidia wanafunzi, wazazi na walezi kuhusu watoto ambao mwanzo walikuwa wamefanya uchaguzi kwa michepuo mingine na kushindwa kupata nafasi.

Jafo amesema Serikali imetafakari na kuona wengi wa wanafunzi wamekuwa wakishindwa kusoma kile wanachokitaka kutokana na kufanya uchaguzi kabla ya matokeo.

“Mfumo huu utakuwa ni suluhisho la malalamiko ya siku nyingi kuhusu machaguo ambayo vijana hufanya kabla ya kushauriana na wazazi wao, lakini wakati mwingine wakishafanya matokeo huja kinyume, sasa watachagua kulingana na ufaulu wao,” amesema.

 Jafo amesema wameamua kutoa fursa hiyo kwa sababu wapo wahitimu wengi walioomba tahasusi ambazo matokeo yalivyotoka hazikuuwiana hivyo kushindwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita.

Waziri huyo amesema wahitimu wa aina hiyo ni wengi na ndio maana Serikali imeamua kuwapa fursa nyingine kuchagua tahasusi upya zinazoendana na matokeo yao ili waweze kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita.

Amesema kazi hiyo itaanza kuanzia terehe 1 mwezi ujao hadi Aprili muda ambao amesema hautaongezwa.

Mtandao wanaotakiwa kuutumia kuomba ni www.selfom.tamisemi.go.tz ambao amesema utakuwa wazi tangu wakati huo.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz