Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliofariki ajalini Pwani wafanyiwa DNA, Muhimbili yawaita ndugu

73801 DNA+PIC

Mon, 2 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam nchini Tanzania imefikia uamuzi wa  kufanya kipimo cha utambuzi wa vinasaba (DNA) kuwatambua watu watano waliofariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea usiku wa kuamkia jana Jumamosi Agosti 31,2019 wilayani Kibiti Mkoa wa Pwani.

Miili ya watu hao wanne wakiwa watu wazima na mmoja mtoto ilifikishwa katika hospitali hiyo jana Jumamosi asubuhi kwa ajili ya kuhifadhiwa ikiwa haitambuliki kutokana na kuharibika.

Taarifa iliyotolewa leo Jumapili Septemba 1,2019 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano MNH, Aminiel Aligaesha imesema miili hiyo imeungua kupita kiasi na kusababisha utambuzi wake kuwa mgumu.

Amesema tayari miili hiyo imefanyiwa  uchunguzi wa awali (postmortem) na kuchukua sampuli kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kitengo cha Forensic Pathology pamoja na Mkemia Mkuu wa Serikali ya Tanzania ili kufanya uchunguzi zaidi.

“Tunawaomba ndugu wa karibu wa marehemu hawa kujitokeza kuanzia kesho (Jumatatu) Septemba 2, 2019 saa mbili asubuhi ili kuchukuliwa sampuli na Mkemia Mkuu wa Serikali.”

“Hiyo itawezesha kusaidia kufanya uchunguzi wa kulinganisha vinasaba kati ya ndugu na marehemu ili waweze kupewa miili hiyo kwa ajili ya mazishi baada ya uchunguzi kukamilika,” amesema Aligaesha

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement   ?
Jana Jumamosi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Onesmo Lyanga akizungumzia ajali hiyo alisema ilihusisha lori la kampuni ya Dangote lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Mtwara likiwa limepakia malighafi ya kutengeneza saruji.

Lori hilo liligongana na gari dogo aina ya Toyota Premio lililokuwa likitoka kwenye nyumba za walimu wa Shule ya Sekondari ya Kibiti eneo la Kinyanya.

Alisema gari hilo liliingia barabara kuu inayotoka Dar es Salaam kwenda Mtwara bila kuzingatia sheria na kugongana na lori hilo.

Kamanda Lyanga alisema  baada ya magari hayo kugongana gari la Dangote lilipoteza mwelekeo na kugonga nguzo ya umeme na nyaya kuanguka iliyosababisha moto ulioshika katika lori hilo na kusababisha vifo vya watu wanne na mmoja kati ya watu wawili waliokuwa katika gari hilo dogo alifariki  wakati akipatiwa matibabu wilayani Rufiji mkoani Pwani.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz