Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliocheza kamari na roho zao Mtwara wasirudie

56274 PIC+KAMARI

Wed, 8 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Watanzania tunaipenda sana siasa, ila baadhi yetu huichomeka pasipostahili. Hata katika mambo yahusuyo maslahi ya umma, au umoja wa wananchi, bado wapo ambao huleta siasa.

Kutokana na habari kuwapo kimbunga Kenneth, baadhi ya Watanzania walilichomeka tukio hilo katika siasa. Wapo waliodhihaki mitandaoni na kuita, “kubeti, uongo, kimbunga hewa, kiki za serikali n.k”. Fikra za namna hii zina athari sana katika jamii.

Ukiwa na watu wanaofikiria kila kitu ni siasa, dhihaka au uongo, ni hatari. Ikiwa maafa yangetokea yangesababisha athari kubwa zaidi.

Siku zote tambua unachoandika husomi peke yako, katika mitandao wengi husoma na hivyo fikra zako zinaweza kuathiri fikra za wengine.

Kule Mtwara, kuna watu walijiona werevu sana, baada ya serikali kuwataka waondoke maeneo hatari, kuna ambao hawakuondoka.

Eti ni werevu huo! Hapana. Ni ujinga wa kiwango cha hatari. Ni sawa na kucheza kamari na roho yako. Hata kama kimbunga hakikutokea kama ilivyotazamiwa, bado ulazima wa kuondoka ulikuwapo.

Tujifunze kwa India, kuhusu kimbunga Fani. Watu zaidi ya milioni moja walihamishwa katika maeneo yao na kweli kimbunga kikayapiga kwelikweli. Ni watu 12 tu waliopoteza maisha, wakiwamo watano walipigwa na radi.

Kimbunga na tetemeko la ardhi ni miongoni mwa majanga ya kimaumbile, hayazuiliki. Lakini upo uwezekano wa kukwepa ili kupunguza maafa makubwa.

Kuna mwandishi mmoja wa habari, alienda Mtwara, akafika hadi ufukweni. Njiani kapishana na makundi ya watu wakielekea maeneo ya kujihifadhi kama ilivyoelekezwa na serikali.

Pale ufukweni, kakutana na mwanaume akiwa na mafungu yake ya dagaa akiendelea na shughuli zake bila wasiwasi. Alipoulizwa kwa nini haondoki na kwenda sehemu salama.

Akajibu kwamba, yeye anamtegemea Mungu, amefanya maombi. Kama kufa mtu atakufa tu, hata akikimbilia wapi.

Unaweza kuwaza kwamba maneno yake yana mantiki. Ni kweli yana mantiki, lakini kayaweka sehemu isiyo sahihi.

Mungu anatuhimiza kusoma. Ili tuwe na uelewa mzuri wa uwepo wake na jinsi ya kumuabudu, pia tuyaelewe mazingira yetu na namna gani tutapambana na changamoto zinazotuzunguka.

Ikiwa elimu imeshatolewa juu ya uwepo wa kimbunga, kisha eti huondoki sehemu hatari kwa kutegemea Mungu. Huo ni ujinga.

Mungu kahimiza tumuombe, na kumtegemea yeye. Wala hakuna anayesema kifo kinakimbilika. Ila ikiwa utaambiwa kuna treni inakuja, ondoka. Usipoondoka ni wazi kwamba una tatizo la kiuelewa kuhusu utendaji kazi wa Mungu. Kwa sababu utakufa kwa ujinga na Mungu atakwenda kukuuliza kwa nini ulikuwa mjinga.

Takribani mwezi mmoja nyuma, Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi, alitangaza siku tatu za maombolezo katika nchi yake kwa vifo vya mamia ya watu kutokana na kimbunga Idai.

Kimbunga kilichozikumba nchi tatu: Msumbiji, Malawi na Zimbabwe. Taarifa zinaeleza mamia ya watu walipoteza maisha.

Ripoti ya mwanahabari wa Aljazeera, Haru Mutasa, ambaye alikita kambi Zimbabwe, ilieleza kuwa Serikali za mataifa hayo, ziliwataka raia wanaoishi maeneo yaliyokuwa na uhakika wa kupigwa na kimbunga waondoke.

Lakini ubishi wao na kumtegemea Mungu vikawaganda vichwani. Wapo waliogoma kuondoka. Wakafa kwa mafuriko, kuangukiwa na mawe na maporomoko ya milima.

Labda tuwaulize wale waliogoma kuondoka Mtwara, kule Msumbuji Mungu hakuwepo? Mbona waliogoma kuondoka walikufa?

Musa alipowachukua wana wa Israel, akaenda nao baharini. Wakati jeshi la Farao linakuja nyuma. Na wao hawana boti wala meli. Alifanya vile kwa sababu alishapewa uhakikisho na Mungu, kwamba aende na yuko pamoja naye. Je, wewe una mkataba wowote na Mungu? Tuache upuuzi!

Kuna kisa maarufu katika ulimwengu wa Kiislamu. Mtu mmoja alimwendea Mtume Muhammad (saw) na malalamiko kwamba ngamia wake kapotea. Alipoulizwa kapotea katika mazingira gani.

Akasema, kamuachia Mungu kisha akaondoka. Hata kumfunga hakumfunga. Mtume akamwambia, hata kama alimtegemea Mungu ila pia alipaswa kumfunga.

Katika mkasa wetu wa kimbunga cha Kenneth, ni sawa na kusema; mtegemee Mungu, fanya maombi ila pia unapaswa kuondoka maeneo hatari.

Ubishi uliofanywa na baadhi ya wakazi wa Mtwara umenikumbusha zile nyakati, serikali inapotangaza ujio wa mvua kubwa, na kuwataka watu wanaoishi mabondeni wahame. Wengi hupuuza, husubiri wahamishwe na mikondo ya mafuriko na upepo mkali.

Hadi tangazo la kimbunga, unaombwa uondoke unagoma. Eti namtegemea Mungu! Hatuna haja ya kumsingizia Mungu kwa kila jambo. Mengine ni ujinga wetu.

Bora uchukue tahadhari hata kama kimbunga hakitotokea. Kuliko kutochukua kisha kikakubananisha. Kimbunga hakiendeshwi na mtu. Muda wowote hubadili kasi au mwelekeo.



Chanzo: mwananchi.co.tz