Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliobomoa makazi kupisha ujenzi sekondari, walia na fiidia

Nyumba Pic1 Data Waliobomoa makazi kupisha ujenzi sekondari, walia na fiidia

Sun, 7 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Wananchi ya Mtaa wa Iduda Kata ya Iziwa jijini Mbeya wamelazimika kubomoa makazi yao kutii agizo la Mkuu wa Wilaya, Dk Rashid Chuachua kwa kile kilochoelezwa kupisha mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari ya kata.

Licha ya kubomoa nyumba zao wenyewe, wananchi hao wamelalamikia kutolipwa fidia ili kupisha eneo hilo.

Wakazi hao wamesema kuwa wameumizwa na kitendo hicho wakidai kuwa makazi yao yamejengwa tangu mwaka 1983 na kwa sasa hawajui wataishi wapi na familia baada ya kubomoa nyumba zao

Stephano Mwasyoge amesema kuwa kitendo cha Serikali kutotoa fidia kimewaweka njia panda na kumwomba Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera kuingilia kati na kuona namna ya kuwasaidia.

"Kwa mfano kama mimi eneo nililojenga lilikuwa la wazazi wangu, nimeishi miaka 45 sasa sielewi naanzia wapi na ntaenda wapi na watoto ambao wanashindwa hata kuhudhuria masomo" amesema Mwasyoge.

Alisema kuwa hawapingani na Serikali kupisha eneo hilo kwa ajili ya mradi wa shule ya sekondari ya kata bali wanaomba kuonewa huruma kutengewa maeneo na kulipwa fidia.

Mjane Laeli Kihobeli amesema anaomba Serikali kuingilia kati na kwamba eneo lake alipanda miti ambayo imekuwa ikikatwa pasipo utaratibu.

Naye China Mazonje amedai kuwa licha ya kumuomba Mkuu wa wilaya kulipwa fidia bado aliwapa siku saba wawe wamebomoa makazi yao na kuwaeleza hakuna fidia.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk Rashid Chuachua amesema ni kweli wameagizwa kubomoa kupisha mradi wa shule ya sekondari ya kata.

Amesema kuwa eneo hilo tangu mwaka 1983 limetengwa kwa ajili ya shughuli za kijamii na suala la fidia hawapaswi kulipwa kabisa.

"Tunavyo vielelezo vyote vya eneo hilo na hakuna aliyeonewa sasa wanapaswa kupisha mradi ambao utakuwa chachu kwa watoto wao kupata elimu bora na eneo hilo idadi kubwa yalikuwa ya wazazi wao"amesema.

Amesema kuwa kaya zinazotakipa kuondoka kwenye eneo hilo ni tano na sio 25 kama baadhi ya watu wanavyodai.

"Kaya zinazotakiwa kuondolewa ni tano tu sio 25 kama madai yao wanavyosema, mwanahabari nenda kajionee mwenyewe pia hakuna mtu atakayelipwa fidia "amesema

Kwa upande wake mwanaharakati wa haki za binadamu, Raphael Ngonde amesema kuwa kitendo cha Mkuu wa wilaya kutoa siku saba bila fidia ni kinyume cha taratibu za sheria za ardhi.

Chanzo: mwananchidigital