Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliobadili matumizi ya ardhi Dar es Salaam kunyang’anywa maeneo yao

87445 Pic+lukuvi Waliobadili matumizi ya ardhi Dar es Salaam kunyang’anywa maeneo yao

Sat, 7 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema ni kosa kisheria kubadilisha matumizi ya ardhi na kwamba, wale waliobadilisha katika Mkoa wa Dar es Salaam watanyang'anywa maeneo hayo.

Lukuvi ameyasema hayo leo Ijumaa Disemba 6, 2019 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza kwenye mkutano wa mashauriano kati ya Serikali, wawekezaji na wafanyabiashara.

Amesema katika Mpango mji wa Jiji la Dar es Salaam wa mwaka 1979, yapo maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda, mengine kwa ajili ya biashara na pia makazi, lakini maeneo hayo kwa sasa hayatumiki kwa malengo kusudiwa.

“Ni kosa kuweka kiwanda kwenye eneo la makazi, wale wote waliobadilisha matumizi ya ardhi, tutawanyang'anya. Eneo la Pugu Road lilikuwa la viwanda lakini sasa watu wamejenga apartment. Ubadilishaji wa matumizi ya ardhi unafuata sheria," amesema waziri huyo.

Lukuvi amesema wako kwenye mchakato wa kuandaa masterplan mpya ya Jiji la Dar es Salaam, amewataka wafanyabiashara kujitokeza kutoa maoni yao kuhusu matumizi ya ardhi ili yawemo kwenye masterplan hiyo kabla haijazinduliwa rasmi.

“Tunatarajia masterplan ya Dar es Salaam iwe imekamilika ifikapo Machi 2020 na kuzinduliwa rasmi, huu ni wakati wenu makundi yote yenye interest kwenye ardhi kutoa maoni yenu,” amesema Lukuvi.

Wakati huohuo, Lukuvi amesema viongozi wa Serikali za mitaa hawana mamlaka ya kupanga matumizi ya ardhi wala kuthibitisha mauzo ya ardhi, hiyo ni kazi ya halmashauri husika.

Hata hivyo, amesema vijiji vinaweza kufanya hivyo kwenye ardhi yao.

Pia, amewataka wapimaji wa ardhi kuhakikisha wanatoa hati kwa wananchi na kuwakabidhi hati zao na kwamba, ikifika Machi 2020 kama hawajafanya hivyo, watafutiwa leseni zao.

Chanzo: mwananchi.co.tz