Wakazi wa vijiji vya Nyenze na Ngwangholo Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga walioathirika kwa tope linalodaiwa kuwa na kemikali kutoka mgodi wa Almasi wa Williamson Diamond Mwadui wamekataa hoja ya kuwataka wahamie eneo la Ukenyenge kwa kile wanachodai uamuzi huo haujawashirikisha.
Msimamo huo umetangazwa jana Jumanne Januari 10, 2023 wakati wa mkutano wa hadhara ulioitishwa kijijini hapo ambao umeshirikisha viongozi wa kijiji na uongozi wa mgodi wa Almasi wa Mwadui.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake ambao nyumba na mashamba yao yaliathiriwa na tope hilo, Revocatus Kurwa ametaja sababu za kukataa hoja hiyo ni uamuzi huo umefikiwa bila wahusika wala uongozi wa kijiji kushirikishwa.
“Baadhi yetu nyumba na mashamba yetu yaliharibiwa kwa kufunikwa na tope na hatuna sehemu ya kuishi wala kulima hadi sasa. Siyo sahihi leo tuambiwe tuhamie kata nyingine bila kulipwa kwanza fidia,” amesema Kurwa
Hoja hiyo iliungwa mkono na Maimuna Kasala, mwananchi mwingine aliyeathirika na tope hilo lililovamia makazi ya watu Novemba 7, 2022 baada ya bwawa la topetaka la mgodi kupasuka na tope hilo kusambaa kwenye makazi na mashamba ya wananchi.
“Tumepoteza mali zetu; tathimini imefanyika na kuahidiwa kulipwa fidia mwezi Desemba, 2022 lakini hadi leo hakuna aliyelipwa na hatujui hatima ya hayo malipo ya fidia; halafu leo tunaambiwa eti tuhamie eneo lingine. Hapana! Uongozi wa mgodi uweke wazi suala hili,” amesema Maimuna
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwangholo, William Bulugu ameungana na wananchi kupinga hoja ya kuwahamishia eneo lingine bila kulipwa fidia wala kushirikishwa maamuzi hayo.
“Hadi sasa hakuna kikao kilichokaa, kujadili na kupitisha makubaliano hayo ya watu kuhamishiwa maeneo mengine zaidi ya kuona taarifa za kuwataka wananchi wahame. Ni vema wananchi washirikishwe kwanza, wakubaliane na kulipwa fidia ndipo suala la kuhamia maeneo mengine lifuate,” amesema Bulugu
Meneja Mkuu wa mgodi wa Williamson Diamond (WDL), Ayubu Mwenda amewatoa hofu wananchi kwa kuwahakikishia kuwa wote walioathirika kwa tope kuingia kwenye mashamba na nyumba zao watalipwa fidia.
Alisema mchakato wa malipo ya fidia hiyo inaendelea na wahusika wataanza kulipwa baada ya tathmini kukamilika.
Kuhusu waathirika kuhamishiwa eneo lingine, kiongozi huyo wa mgodi amesema vikao vya makubaliano na uamuzi vitakavyoshirikisha wote wanaohusika vitafanyika kwa lengo la kupata maridhiano ya pamoja kati ya pande zote.