Waathirika wa mafuriko katika mtaa wa Iwambala Kata ya Uyole jijini Mbeya wamesema hawajajua hatma yao kutokana na kukosa makazi, chakula na mavazi baada ya mali zao kusombwa na maji.
Wametoa kilio chao leo Jumanne, Januari 10, 2023 wakizungumza na Mwananchi Digital ilipotembelea makazi yao kushuhudia mafuriko yaliyowakumba kufuatia mvua iliyonyesha siku mbili zilizopita na kuwaachia maumivu.
Julius Mwambenja na mke wake, Halima Julius wamesema kwa sasa hawana chakula na mavazi baada ya mvua kusomba vitu vyote ndani huku nyumba pia ikiwa imejaa maji na tope.
"Serikali itusaidie chakula, hata pakulala hatuna, unaona tulipo utadhani ni ziwani tunaelea tu juu juu, hatuna kazi tunaishi kwa vibarua" amesema Julius.
Naye Joyce Kajula, mwenye watoto saba amesema mvua iliyonyesha Jumamosi haikuacha kitu ndani zaidi ya maji na tope na kwamba upo uwezekano wa njaa kuwaua na watoto wake kushindwa kwenda shule.
"Jumla tupo nane, angalia nyumba ilivyo jaa tope hatuna pakulala, chakula hakuna sijala tangu jana, wanafunzi vifaa vyao vya shule vimesombwa na maji nakosa cha kufanya, serikali ituangalie," amesema Joyce huku akitokwa na machozi.
Kwa upande wake, Wambi Njango amesema mafuriko hayo yamewaachia hasara kwani hakuna kilochobaki ndani zaidi ya maji huku chakula, mavazi na vitu vingine vikisombwa.
"Nina wanafunzi wa darasa la sita, la nne na la kwanza vifaa vyao vyote hakuna kilichobaki, tunashukuru kwa msaada wa chakula cha jana kutoka kwa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson japokuwa hatujui leo, kesho na huko mbeleni itakuaje," amesema.
Akizungumzia tukio hilo, Diwani wa eneo hilo, Daniel Njango amesema mafuriko hayo ni ya pili kwa ukubwa tangu yale ya mwaka 1982.
"Tunapambana kuwatafutia makazi kwa majirani, watu 162 ndio waliathirika na kaya tisa hazina makazi, mifugo zaidi ya 1000 imeenda na maji," amesema Njango.