Lindi. Walinzi wa shule za msingi za manispaa ya Lindi wanalalamikia kitendo cha kutolipwa mishahara yao kwa muda wa zaidi ya miezi 10 hadi sasa.
Malalamiko hayo yametolewa na uongozi wa walinzi hao wakati walipokuwa wanazungumza na Mwananchi ofisini kwao.
Salumu Abdallah, mwenyekiti wa walinzi hao alisema halmashauri ya manispaa mwaka 2010 iliajiri walinzi 31 wa shule za msingi kwa mikataba ya muda mrefu
Abdallah alisema tangu mwaka 2010 baada ya kupata ajira hizo malipo ya mishahara yao yamekuwa ya kusuasua hadi kufikia hatua ya kutolipwa kabisa.
Alisema jumla ya shilingi milioni 17 ambayo ni mishahara ya miezi 10 haijalipwa hadi sasa hali inayosababisha walinzi hao kukosa morari ya kufanya kazi.
“Unajua maisha yetu yamekuwa magumu sana kwa sasa kwani tegemeo letu ni kazi yetu ya ulinzi,’’ alisema mwenyekiti huyo.
Kajura Robert alisema kitendo cha kutolipwa mishahara yao kinakwamisha kufanya shughuli zao za maendeleo ikiwemo kuhudumia familia na watoto wa shule
Ofisa elimu shule za msingi manispaa ya Lindi, Husseni Kitingi amekiri kuwepo kwa deni la walinzi kutokana na kuwepo sheria ya elimu bure inayozuia wazazi kuchangia elimu.
Kitingi amewaomba walinzi hao kuwa wavumilivu wakati halmashauri ikihangaika kutafuta fedha kwa ajili ya malipo ya deni hilo ambalo litapunguzwa kulingana na hali ya kiuchumi itakavyoruhusu