Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walimu watakiwa kutafuta mbinu mbadala

21314 Waalim+pic TanzaniaWeb

Tue, 9 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Wito umetolewa kwa walimu kutafuta mbinu mbadala  za ufundishaji ili kuwasaidia wanafunzi kufanya vizuri kwenye masomo yao.

Wito huo umetolewa leo Oktoba 7, 2O18 na Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Dar es salaam, Maimuna Mtanda wakati wa mahafali ya 11 ya darasa la saba Shule ya Msingi Heritage iliyoko Ilala, Dar es Salaam.

Amesema njia mbadala zitakazotumiwa zitawasaidia wanafunzi kujenga uelewa hasa tunapoelekea uchumi wa viwanda.

"Nimefurahishwa na mbinu zinazotolewa za wanafunzi kujisomea, kwanza zinawasaidia kupata uelewa zaidi lakini tunapoelekea uchumi wa viwanda zitawasaidia kuwa wabunifu," amesema Mtanda.

"Nimekuwa nikitembelea shule mbalimbali lakini hii imekuwa tofauti, nimeona mabanda yanayotumiwa na wanafunzi kuongeza mbinu za kujifunza," amesema.

Mkuu wa shule hiyo, Magabe Kimori amewataka wanafunzi waliohitimu kuzingatia maadili waliyofundishwa na kuwa na nidhamu shule watakazokwenda kuendelea kidato cha kwanza.

"Shule hii inafundisha kwa vitendo lakini kikubwa ni nidhamu kwa wanafunzi, tunatamani yote tunayoyafundisha wakayaendeleze huko waendako," amesema Kimori.

Amesema kunapotokea mabadiliko yoyote wamekuwa wakitoa semina  kwanza kwa walimu ili kuendana na mfumo utakaotakiwa kwa wakati huo.

Akiongea kwa niaba ya wahitimu, Secilia Sebastian ameiomba Serikali kutafuta suluhisho la vitabu na machapisho yanayokinzana katika kueleza na kufafanua mada mbalimbali.

"Tunaziomba mamlaka husika kuona namna nzuri ya kutoa mkanganyiko unaojitokeza katika vitabu na machapisho mbalimbali" amesema Secilia.

Katika mahafali hayo jumla ya wanafunzi 88 wa darasa la saba  wamehitimu na kukabidhiwa vyeti katika mtihani uliofanyika Septemba 5 na 6 mwaka huu.

Chanzo: mwananchi.co.tz