MKUU wa Mkoa Mtwara, Gelasius Byakanwa (pichani), amewataka walimu kutumia vema mafunzo kuhusu nidhamu ya fedha na uwekezaji, ili kuepuka ukopaji usio na malengo wala tija.
Katika Siku ya Walimu na Benki iliyofanyika mwishoni mwa wiki, ikiwa na kaulimbiu: ‘NMB na Walimu – Hatua kwa Hatua’, Byakanwa alisema utafiti aliofanya unaonesha walimu wengi wamekuwa na utitiri wa mikopo isiyo na malengo wala tija, hivyo uwepo wa makongamano kama hayo utamaliza changamoto hiyo.
Aliwataka washiriki kutumia kongamano hilo kwa kujielimisha, lakini pia kushauri mambo yanayoweza kufanywa na benki hiyo ili kuharakisha maendeleo.
“Kumbukeni kuwa haya yanayofanywa na NMB yanaunga mkono juhudi za Serikali ya Rais John Magufuli za kuwaunganisha Watanzania katika mifumo rasmi ya huduma za kibenki.
Nyinyi ni kati ya watu mnaoongoza kwa mikopo isiyo na tija kwenu, hili ni jukwaa linaloenda kuwabadili iwapo mtatumia vema elimu hii,” alisema.
Meneja Mwandamizi wa Wateja Binafsi na Kati wa NMB, Ally Ngingite, aliahidi kwa Mkuu wa Mkoa kuwa, benki hiyo iko imara kusambaza elimu ya nidhamu ya fedha na kuwaepusha wateja katika ukopaji hasi.
“Fahari ya NMB siyo tu kukopesha walimu wanaotaka mikopo ama makundi mengine ya wakopaji katika jamii, bali kupata wakopaji wenye malengo na maono ya fursa za kumnufaisha mkopaji mmoja mmoja, taifa na benki yetu.
Hii ndio siri na lengo letu kuyapa elimu makundi haya,” alisema Ngingite. Alibainisha kuwa NMB ambayo kwa sasa ina wateja zaidi ya milioni 3.2, kati yao milioni 2.5 wameunganishwa na huduma za kidijitali.
Meneja wa NMB Kanda ya Kusini, Janeth Shango, aliwapongeza walimu wanaofundisha mkoani Mtwara kwa kuuwezesha mkoa huo kushika nafasi ya pili kitaifa katika matokeo ya ufaulu wa kidato cha sita.
“Kufanya kwao vema darasani kunatokana na utulivu wanaopata kupitia elimu na mafunzo wanayopatiwa na NMB,” alisema na kuunga mkono kauli ya Byakanwa kuwa, kuna ukopaji usio na malengo wala tija kwa walimu wengi na makundi mengine.
Aliahidi kuendeleza kasi waliyo nayo katika kutoa elimu kwa makundi yote kwenye jamii, hususani walimu. Wakizungumzia mafunzo waliyopata katika kongamano hilo, washiriki walikiri kauli ya Byakanwa kuhusu uwepo wa walimu wanaokopa kabla ya kufikiria malengo ya ukopaji.
Mwalimu Sophia Luani wa Shule ya Msingi Tandika iliyopo Manispaa ya Mtwara, alisema walimu ni kati ya vinara wa ukopaji usio na tija na anaamini elimu waliyopewa itawajengea fikra mpya katika kila mradi, biashara ama ujasiriamali watakaouanzisha.