Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walimu waliofaulisha kidato cha sita kupewa viwanja

81016372ef48c1d54104886710850eea.jpeg Walimu waliofaulisha kidato cha sita kupewa viwanja

Wed, 14 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MKUU wa Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Lazaro Twange atawakabidhi viwanja walimu 46 wa Shule ya Sekondari ya Dareda, ikiwa ni motisha kutokana na wanafunzi wa shule hiyo kufanya vizuri katika mitihani ya taifa ya kidato cha sita.

Katika matokeo ya mitihani hiyo ya mwaka 2020/2021, shule hiyo ilishika nafasi ya tatu kitaifa kati ya shule 610.

Walimu wa shule hiyo ambayo ni ya kwanza kimkoa kati ya shule 19 za sekondari mkoani Manyara, pia wamepewa fursa ya kutembelea hifadhi mbili za taifa. Shule hiyo ilikuwa na watahiniwa 101 kwenye mitihani hiyo ya kidato cha sita.

Kwenye kikao kilichohudhiriwa na walimu wa shule hiyo na viongozi wa serikali za vijiji vinavyounda kata ya Dareda, Twange alisema kabla ya mwezi huu kumalizika, atakabidhi viwanja kwa walimu hao.

Wakati wa mkutano huo, walimu hao waliomba kutembelea hifadhi za taifa hasa zilizopo mkoani Manyara.

"Nitakuwa mkuu wa wilaya wa ajabu sana kama nikishindwa kuwapa fursa ya kwenda kutembelea hifadhi, nitauza hata koti langu kwa hiyo niwahakikishie nyie andaeni utaratibu na idadi na siku mnayotaka kutembelea nitafanya utaratibu mara moja mtembelee hifadhi hizo," alisema Twange.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Babati Vijijini, Jackson Haibei alitoa Sh 200,000 kuwapa walimu wa shule hiyo kuwapa motisha na ari ya kufundisha kwa ari zaidi.

"Kwa kweli niwapongeza Dareda kwa hatua hiyo mliyofikia na sisi kama chama tumeona tuwashike mkono kwa kuwapa Sh 200,000," alisema Haibei na kuhimiza ushirikiano wa wananchi kwa walimu na uongozi wa shule.

Walimu wa Shule ya Sekondari Dareda waliishukuru serikali kwa motisha ya viwanja na kueleza kwamba itakuwa changamoto kwao kuzidisha bidii ili ishike nafasi ya kwanza kitaifa.

"Mimi kama mwalimu kijana kwanza niishukuru serikali kwa kutupa viwanja hasa sisi ambao hatukuwa na viwanja kwa ajili ya ujenzi ila tunaichukua kama changamoto na fursa ya kutufanya tuongeze bidii zaidi ili tushuke nafasi ya kwanza badala ya nafasi ya tatu kitaifa kama sasa," alisema mwalimu, Anna Lucas.

Mkuu wa Taaluma katika shule hiyo, Lazaro Nairowa aliiomba jamii iwape ushirikiano ili wafanye vizuri zaidi.

Mkuu wa shule hiyo, Joel lazier alisema ingawa wamefanya vizuri, lakini wanakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwamo wanasiasa kuingilia taaluma.

Alisema changamoto nyingine ni ukosefu wa maji shuleni hapo hali inayowalazimu baadhi ya wanafunzi hukosa vipindi kwa ajili ya kutafuta maji, upungufu wa mabweni na kukosa uzio kuzunguka shule.

Chanzo: www.habarileo.co.tz