Dar es Salaam. Walimu wa madarasa ya awali wametakiwa kuwafanya watoto rafiki zao ili iwe rahisi kuelewa kile wanacho wafundisha darasani.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Prestige jijini Dar es Salaam, Ajira Hongoli amesema hayo baada ya kumaliza mafunzo ya elimu ya awali yanayoitwa ‘mwanzo mzuri’ ambayo yametolewa kwa ushirikiano baina ta Taasisi ya Haki Elimu, Chuo Kikuu cha Mkwawa na Chuo Kikuu cha Via cha nchini Dermark.
“Tuwafanye watoto rafiki zetu, tujifunze kutoka kwao nimeweza kufanya hilo ninaloongea baada ya kupata haya mafunzo, sina mtoto anayeniogopa kwenye darasa langu, wote wamekuwa rafiki zangu,” amesema Hongoli.
Mkurugenzi Mtendaji wa Haki Elimu, Dk John Kalage amesema mafunzo hayo yamelenga kuwaongezea walimu hao ujuzi baada ya tafiti mbalimbali kuonyesha watoto wasipopata elimu ya awali hawawi na mwanzo mzuri wa kujifunza.
Dk Kalage amesema wanatarajia kuwafikia walimu kutoka shule 127 za Serikali na binafsi ili matokeo ya watoto kujifunza yasaidie kuendelea kuandaa mbinu bora za kujifunza.
“Mafunzo haya ni kama utafiti tunataka kuona matokeo ya shule ambazo walimu wamefundishwa mbinu bora za kuwafundisha watoto kutoka kwenye mradi huu wa mwanzo mzuri,” amesema Dk Kalage.
Pia Soma
- Hotuba ya Kabudi UN yaibua mjadala
- Mchungaji awataka wazazi kushirikiana na walimu katika maswala ya maadili
- Diamond ashindwa kupanda Mlima Kilimanjaro, Steve Nyerere azitema Sh2 milioni
“Tunachotaka ni kuona ubora wa elimu kwenye nchi yetu ya Tanzania, tunaamini walimu wakishirikiana katika kubadilishana uzoefu na kupewa mafunzo, ubora wa elimu utaongezeka,” anasema.
Naye Mratibu wa Chuo Kikuu cha Via nchini Tanzania, Dk Suma Kaare amesema zipo mbinu za kumfanya mtoto apende shule na aelewe masomo darasani, na hizo ndizo walizokuwa wanafundisha.
“Elimu ya awali inamtengeneza mtoto kuwa sehemu ya dunia, inampa mwanzo mzuri wa masomo yake na walimu wanaofundisha lazima wawe wamenolewa kuweza kutoa elimu hiyo kwa watoto,” amesema Dk Kaare.