Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walimu, asasi zaagizwa kuwezesha haki kwa watoto walemavu

A054aaacaf322ade1a7495e997f2ef42.jpeg Walimu, asasi zaagizwa kuwezesha haki kwa watoto walemavu

Wed, 9 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Bahi mkoani Dodoma, Fatuma Mganga, amewaagiza walimu kushirikiana na asasi za kiraia kwa lengo la kufichua watoto wenye ulemavu waliofichwa ili wapate haki zao ikiwamo elimu.

Mganga alisema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya mradi wa elimu jumuishi yaliyojumisha walimu wa wilaya hiyo.

Alisema walimu wana wajibu mkubwa katika kushirikiana na asasi ambazo zimekuwa msaada mkubwa kwa kuwaibua watoto wanaokosa haki zao za kimsingi kwa kufichwa majumbani.

Pia aliwataka walimu waliopewa mafunzo kutumia fursa ya elimu walioipata kufanya kazi kwa vitendo ili wawasaidie kupata mbinu zaidi.

Mratibu wa mradi huo wilayani Bahi, Jenni Mgidange, alisema bado kuna wazazi na walezi wanaofikiri kumsomesha mtoto mwenye ulemavu ni hasara na ndiyo maana mpaka sasa kuna wazazi wanowaficha watoto wao majumbani.

Alisema kutokana na imani hiyo iliyojengeka kwa wazazi, walezi na jamii, imewafanya watoto wenye ulemavu waliopo majumbani kuendelea kuwa masikini.

Mgidange aliwasihi walimu kuhakikisha wanafunzi wenye ulemavu wanafanya vizuri kitaaluma ili wafikie malengo yao na kuondokana na umasikini.

Naye Dk Wakuru Manini wa Chuo cha Ualimu Patandi, aliwasihi walimu kuwa karibu na watoto wenye ulemavu wakati wote wakiwa ndani au nje ya darasa.

&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&

TMA yaandaa warsha kwa wachimbaji madini wadogo

Na Anastazia Anyimike

MATUMIZI sahihi ya taarifa za hali ya hewa yatasaidia kuongeza tija, ufanisi na usalama katika shughuli zinazohusiana na utafutaji, uchimbaji wa madini na uendeshaji wa migodi.

Hayo yalisemwa na Aron Kisaka aliyemwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi akifungua warsha ya wachimbaji wadogo iliyoandaliwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Kisaka alisema kutokana na kukosekana kwa taarifa za hali ya hewa kwa wachimbaji, imekuwa chanzo cha kuhatarisha usalama wa wachimbaji wa madini hususani wachimbaji wadogo.

Alisema Mamlaka inatambua kuwa utekelezaji wa sheria katika sekta ya madini utasaidia kupunguza madhara yanayotokana na matukio ya hali mbaya ya hewa migodini kwa kutumia taarifa mahususi na sahihi za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Warsha hiyo iliyoandaliwa na TMA ililenga kujenga uelewa wa pamoja kwa wadau kuhusu Sheria Na 2 ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na itashirikisha washiriki kutoka sehemu mbalimbali ikiwemo Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Wizara ya Madini, Tume ya Madini , wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dk Agnes Kijazi, alisema Mamlaka yake inatoa huduma mahususi kwa ajili ya sekta mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na sekta ya madini.

Dk Kijazi alisema wadau katika sekta ya madini bado hawazitumii ipasavyo huduma hizo.

Alisema warsha hiyo ni fursa muhimu ya kujengeana uelewa kuhusu umuhimu wa huduma za hali ya hewa katika sekta ya madini na faida zitakazopatikana endapo huduma hizi zitatumiwa ipasavyo.

Naye Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Nchini (FEMATA) na Kamishna kutoka Tume ya Madini, Haroun Kinega, alisema wadau wa sekta ya madini wanahitaji taarifa za hali ya hewa zilizo sahihi na za wakati ili wawe salama, wazalishe kwa tija na kuchangia uchumi.

“Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Robert Sunday, alisema ili sekta ya madini iendelee kuchangia katika uchumi na Pato la Taifa, ni vyema usalama wa watu ambao ni zaidi ya 300,000 walioajiriwa na sekta ya madini kuwa salama na mali zao.

Chanzo: habarileo.co.tz