Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walimu Makete watakiwa kuoa ili kuepuka tamaa kwa wanafunzi

Makete (600 X 355) Walimu Makete watakiwa kuoa ili kuepuka tamaa kwa wanafunzi

Sat, 23 Oct 2021 Chanzo: mwananchidigital

Walimu wa shule za sekondari wilayani Makete mkoani Njombe wametakiwa kuoa ili kupunguza tamaa ya kimapenzi na wanafunzi na kuwasababishia kupata ujauzito.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi Oktoba 23, 2021 na Mkurugenzi Mtendaji wilaya hiyo, Willium Makufwe wakati akipokea msaada wa mifuko 100 ya saruji iliyotolewa na shirika la nyumba la taifa (NHC) kwa shule ya sekondari Lupila iliyopo wilayani humo.

Amesema wapo baadhi ya walimu waliokosa maadili wamekuwa wakiwarubuni wanafunzi ili kufanya nao mapenzi hali inayosababisha kupata mimba na ndoto zao kupotea.

Alisema walimu wanatakiwa kuwa mfano mzuri kwa jamii kwa kuhakikisha wanawafundisha wanafunzi maadili yaliyo mema ili wanapomaliza masomo yao wakaishi vizuri huko waendapo.

"Tunataka mwalimu afanye kazi kwa uadilifu, uaminifu na bahati mbaya mwalimu ni mlezi hatutaki kesi eti mwalimu anashiriki katika kuharibu maisha ya mwanafunzi hasa wa kike," amesema Makufwe.

Amesema zipo kesi kama hizo za walimu kuwapa mimba wanafunzi na zimetokea katika shule zingine lakini katika wilaya ya Makete hataki kusikia hilo limetokea.

Alisema Serikali imetoa Sh40 milioni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili shuleni hapo na kuwasihi viongozi kuzisimamia vyema na atakayebainika kufuja pesa hizo hatovumiliwa.

Diwani wa kata ya Lupila Ernesta Lwilla pamoja na kuishukuru serikali kwa kutoa fedha hizo amemuomba mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo kuona namna ya kuwasaidia kupata watendaji wa vijiji vinne kwenye kata hiyo ya Lupila.

"Kata yetu ina changamoto ya kutokuwa na watendaji katika vijiji vinne vya Kijombo, Ukange, Ludilu na Igumbilo ambaye hajui kutumia POS," amesema Lwila.

Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mkoa wa Mbeya, Ramadhan Macha amesema shirika hilo limetoa msaada huo wa mifuko 100 ya saruji kwa shule hiyo kutokana na maombi ya Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Njombe Neema Mgaya aliyoyatoa kwa mkurugenzi mkuu wa NHC, Maulid Banyani.

Chanzo: mwananchidigital