Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walichokisema wafanyabiashara wadogo Dar matumizi mifuko mbadala

60843 Pic+makamba

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba akitembelea maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam kukagua siku ya kwanza ya matumizi ya mifuko mbadala, baadhi wafanyabiashara katika maeneo ya Jiji hilo wameeleza changamoto za matumizi ya mifuko hiyo.

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Juni Mosi, 2019 wamesema mifuko mbadala si rafiki kwa kubeba samaki, kuku aliyechinjwa na mboga za majani.

Abdi Othman, muuza samaki katika soko la Feri amesema mifuko hiyo inavujisha maji ambayo baadaye hutoa harufu mbaya.

“Mifuko hii mbadala inaoza lakini kwa samaki siyo rafiki kwa sababu inavujisha maji, angalau isivuje inabidi tumfungie katika mifuko miwili au mitano na kumbuka kuwa mfuko mmoja unauzwa Sh500,” amesema Othman.

Ameiomba Serikali kueleza matumizi ya mifuko mbadala  ambayo ni rafiki kwa kubeba bidhaa zenye maji kama samaki na nyama.

Amesema mifuko mbadala ni mizuri zaidi kwa kubebea bidhaa nyingine ambazo hazina maji.

Habari zinazohusiana na hii

Mkazi wa Gongo la Mboto,  Amri Sharifu amesema mifuko hiyo mbali na kuuzwa bei ghali haina ubora.

“Tumeumizwa mfuko kama huu (huku akiuonyesha)  ni Sh1,000 lakini hautoshi kubeba mzigo wote nalazimika kuwa na mifuko miwili wakati awali ile ya plastiki tuliuziwa kwa Sh200amesema Sharifu, mchuuzi wa samaki katika soko la Feri.

Naye Rashid Sultan amesema mifuko hiyo si imara na inapitisha damu na majimaji jambo alilodai kuwa kero kwa wateja.

Amesema katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki linapaswa kutazamwa upya, akishauri itumike katika bidhaa ambazo ubebaji wake kwa kutumia mifuko mbadala huleta kero.

“Kwa kawaida mtu akija kuchukua kuku huwa tunamchinjia kabisa na kumuwekea katika mfuko lakini kwa mifuko hii mbadala changamoto ni kubwa, lakini pia ina gharama kubwa,” amesema.

Muuza mboga za majani katika soko hilo, Salome Katininda amesema, “Mboga za majani zinakuwa na maji na huwezi kumshikisha mtu mkononi, ninachofanya tangu asubuhi ya leo nawawekea kwenye mifuko ya karatasi,”

Chanzo: mwananchi.co.tz