Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walichoahidi Hapi, Chalamila kwa wananchi wa Iringa, Mbeya

10499 Hapi+pic TanzaniaWeb

Tue, 7 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Iringa/Mbeya. Wakuu wapya wa mikoa ya Iringa na Mbeya wamekabidhiwa ofisi, huku wakiainisha mikakati yao ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi akizungumza na watumishi jana alisema katika utendaji wake anachokiamini ni ukweli, haki na uadilifu.

Aliwataka watendaji wa Serikali kuwaheshimu wananchi katika utumishi wao na kuheshimu sheria za nchi ikiwa ni pamoja na mipaka yao ya kazi.

“Nitasimamia sheria na nitashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa na kuhakikisha wananchi hawatoi rushwa katika utendaji wa Serikali ili watatuliwe changamoto zao,” alisema Hapi.

Alitaja vipaumbele vyake katika utendaji kuwa ni ulinzi na usalama; kukusanya mapato ya Serikali kwa kuibua vyanzo vipya; kusikiliza kero za wananchi na kuwashughulikia watumishi watakaozalisha chuki na Serikali.

Hapi alisema kila mtumishi atapaswa kujitathmini kiutendaji na atahakikisha kila halmashauri inatoa asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kukopesha wajasiriamali na kuhakikisha huduma za jamii zinazidi kuboreshwa na usimamizi unakuwa wenye tija.

Alimpongeza mtangulizi wake, Amina Masenza na katibu tawala anayeondoka, Wamoja Ayubu kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Hapi aliomba ushirikiano ili kusukuma kwa kasi kubwa zaidi gurudumu la maendeleo.

“Ninachosisitiza katika utendaji wa kazi ni ushirikiano kati ya watumishi na kikubwa ni kuondoa migogoro isiyo ya lazima ili kutekeleza mahitaji ya wananchi na kuondoa kero zinazowakabili,” alisema

Katika kukabidhi ofisi, Masenza alimpatia mrithi wake taarifa ya maendeleo ya mkoa inayojumuisha mafanikio na changamoto.

“Nakukabidhi ofisi hii utaanzia pale nilipoishia katika utekelezaji wako kwa wananchi na hata kama kuna mahali sikufanikiwa kufanya vizuri ni vyema ukarekebisha kwa faida ya wananchi na si kuacha kutekelezwa kwa sababu fulani alishindwa,” alisema.

Awali, Hapi alijitambulisha katika ofisi za CCM mkoani Iringa ambako alipokewa kaimu mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Salim Asas ambaye alimkabidhi ilani ya chama hicho akisisitiza umuhimu wa watendaji wa Serikali kuitekeleza kwa vitendo ili kuwapunguzia malalamiko wapiga kura na wananchi kwa jumla.

Mapato Mbeya

Albert Chalamila, ambaye naye alikabidhiwa ofisi jana kuongoza Mkoa wa Mbeya alisema atafanyia kazi suala la kushuka kwa mapato ya Jiji la Mbeya.

Akizungumza mbele ya viongozi waandamizi wa mkoa, wilaya na wananchi waliohudhuria makabidhiano hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mkapa, Chalamila alisema walipoapishwa na Rais John Magufuli walipewa miongozo ya kuifanyia kazi.

“Jiji la Mbeya lilitajwa na Rais jinsi linavyolegalega katika ukusanyaji wa mapato. Ni ujumbe ambao lazima tukae kwa pamoja tutafakari hoja hiyo na njia sahihi za kukabiliana na hali hii,” alisema.

Chalamila aliomba ushirikiano wa dhati kwa viongozi wa ngazi zote na wananchi lakini akatoa angalizo kuwa yeye si mtu wa kuyumbishwa na hataki kufananishwa na mtu yeyote katika utendaji, hivyo aachwe atekeleze majukumu aliyopewa na Rais.

Akikabidhi ofisi hiyo, Amos Makalla ambaye sasa ni mkuu wa Mkoa wa Katavi alisema alifanikiwa kutatua changamoto kwa kushirikiana na wananchi lakini akasema kuna mambo ambayo hayajakamilika akiyataja kuwa ni migogoro ya ardhi ukiwamo wa mipaka kati ya baadhi ya vijijini wilayani Mbarali na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Pia, hifadhi ya Kitulo na wananchi wa vijiji vinavyoizunguka; Kijiji cha Ilolo Katani Kiwira wilayani Rungwe na Kanisa la Moravian Tanzania.

Makabidhiano hayo yalienda sambamba na kuapishwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Maryprisca Mahundi.

Baada ya kiapo, Mahundi alisema, “Nikuhakikishie mkuu wa mkoa na wananchi wa Chunya, mimi si kiongozi wa kuwekwa mfukoni. Nitakwenda kuhakikisha amani, utulivu, haki na maendeleo yanakwenda kutekelezeka kwa masilahi ya Chunya na Mkoa wa Mbeya.”

Imeandikwa na Berdina Majinge (Iringa), Godfrey Kahango na Ipyana Samson (Mbeya) na Haika Kimaro (Mtwara).

Chanzo: mwananchi.co.tz