Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walalamikia bei kubwa ya maji

B20aa8c3032de3ed730142ec3c474f5c Walalamikia bei kubwa ya maji

Mon, 1 Mar 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WANANCHI wilaya Kakonko mkoani hapa wamelalamikia bei kubwa ya maji, huku wengi wakitaka iwe bila malipo.

Hayo yalisemwa juzi na Meneja wa Mamlaka ya Maji Mijini na Vijijini (Ruwasa) wilaya Kakonko, Benjamen Bryton wakati akitoa taarifa kwenye kikao cha wadau wa maji wa wilaya hiyo.

Alisema hali hiyo inachangia kuifanya miradi mingi kutokuwa endelevu.

Bryton alisema wananchi wengi wanataka bei ya ndoo moja ya maji ya lita 20 kuwa Sh 10 au kutolewa bure wakipinga bei ya sasa ya Sh 25 na 20 kwa ndoo ya lita 20 jambo ambalo likitekelezwa linaathiri uendeshaji wa miradi ambapo kwa sasa kuna idadi ndogo ya wateja wanaotumia huduma ya miradi hiyo kutokana na kukwepa gharama hivyo kushindwa kufikia gharama za uendeshaji.

Kutokana na hali hiyo, alisema uhamasishaji unapaswa ufanywe ili kuwaelewesha wananchi umuhimu wa kuchangia huduma ya maji ili kuifanya miradi hiyo kuwa endelevu ns sheria ndogo zinazosimamia uendeshaji wa miradi hiyo zinapaswa kufuatwa.

Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji alisema hali ya upatikanaji wa maji wilaya ya Kakonko imeongezeka kutoka asilimia 48 Januari mwaka jana na kufikia asilimia 73 Januari, mwaka huu kutokana na kukamilika kwa utekelezaji wa miradi ya maji kwenye vijiji 30.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya Kakonko, Hosea Ndagala alisema uchangiaji wa huduma ya maji kwa wananchi ni sera ya serikali, hivyo wananchi wote wanapaswa kuitekeleza ili kuifanya miradi hiyo kupata fedha za ukarabati wa miundombinu ya maji inapoharibika.

“Lazima viongozi wa vijiji na kata kwa kushirikiana na wataalamu wa Ruwasa Kakonko wafanye kazi ya ziada kutoa elimu na kuhamasisha jamii umuhimu wa uchangiaji huduma ya maji kwenye maeneo yao, vinginevyo miradi itaharibika na kuwafanya kukosa huduma hiyo kabisa,” alisema.

Aliwataka viongozi wa vijiji na madiwani kuacha siasa, badala yake watumie nafasi zao kusimamia maelekezo ya serikali hasa undeshaji wa miradi ya maji ambayo serikali imetumia gharama kubwa kuitekeleza, lakini pia kuhakikisha wananchi wanachangia huduma hiyo.

Baadhi ya wadau waliohudhuria mkutano huo akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji cha Churazo, Lucas Elias wameitaka serikali iangalie upya gharama ya huduma ya bei ya maji kwani ya sasa ya Sh 20 kwa ndoo ya lita 20 ni kubwa na wananchi hawawezi kuimudu.

Chanzo: habarileo.co.tz