Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakwapua mali za wagonjwa wodini

48660 Wakwapuapic

Tue, 26 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Jana alfajiri wagonjwa waliolazwa wodi ya Hospitali ya Kilimanjaro CRCT walijikuta katika taharuki baada ya watu wawili kuingia na kupora mali zao.

Watu hao waliingia wodi namba moja saa 11:00 alfajiri na wagonjwa walidhani kuwa ni madaktari waliofika kumsaidia mmoja wao aliyekuwa amezidiwa, kwa mujibu wa daadhi ya wagonjwa walioongea na Mwananchi.

“Walipoingia mmoja alisimama mlangoni na mwingine akaingia ndani,” alisema mmoja wa wagonjwa hao, Akwilina Venance.

“Lakini ghafla tukaona huyu aliyeingia ndani akachukua simu mbili zilizokuwa kwenye chaji kisha akachukua zilizokuwa kitandani.”

Alisema baadaye mtu huyo alianza kukusanya pochi za wagonjwa.

“Ndipo tukashtuka kuwa hawakuwa madaktari bali wezi. Tukaanza kupiga kelele,” alisema.

“Mimi nilisimama nikiwa na dripu mkononi. Kuona hivyo wakatoka na kukimbilia kwenye uzio wakaruka nje.”

Mtu mwingine aliyekuwa akimsaidia mgonjwa wake ambaye amelazwa, Rebeca Msigiti alisema watu hao walichukua simu tatu za mkononi na pochi zilizokuwa na fedha, vitambulisho na nyaraka nyingine.

“Watu hao ni vibaka. Bahati mbaya tuliposhtuka kuwa ni wezi tayari walikuwa wameshabeba vitu hivyo baada ya kushtukiwa na mgonjwa mmoja aliyenyanyuka na kupiga kelele,” alisema Rebeca.

Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Prosper Maro hakuwa tayari kueleza chochote kuhusu tukio hilo kwa maelezo kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi.

“Polisi wapo wanafanya uchunguzi, sina cha kuongea kwa sasa mpaka wamalize uchunguzi wao,” alisema.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alisema wameshaanza msako ili kubaini mtandao wa watu waliojihusisha na uhalifu huo.

“Ni kweli jana waliingia vibaka wawili katika moja ya wodi za Hospitali ya Kilimanjaro,” alisema Kamanda Issah.

“Mmoja alisimama mlangoni na mwingine akaingia ndani, waliiba fedha taslimu na pochi.”



Chanzo: mwananchi.co.tz