Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakuu wapya wa wilaya wapewa somo

9716 WAKUU+PIC TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Waliokuwa wakuu wa wilaya za Nyamagana, Ilemela na Magu wamewapa siri ya mafanikio warithi wao wakiwataka kushirikiana na watumishi walio chini yao, jamii inayowazunguka pamoja na kumtanguliza Mungu mbele.

Wametoa kauli hiyo leo Alhamisi Julai 2, 2018 wakati wakizungumza katika hafla ya kuwaapisha wakuu wapya wa wilaya hizo.

Wakuu wa wilaya waliomaliza muda wao ni Mary Tesha (Nyamagana), Dk Leonard Masele (Ilemela) na Khadija Nyembo wa Magu.

Wamesema ushirikiano miongoni mwa viongozi na wadau ndio siri ya mafanikio katika kutekeleza majukumu na miradi ya maendeleo.

Wakati Nyembo na Dk Masele wakistaafu utumishi wa umma, Tesha  aliachwa katika uteuzi uliotangazwa Julai 28, 2018 na Rais John Magufuli.

Akisisitiza umuhimu wa ushirikiano, Nyembo aliyetumika nafasi hiyo kwa miaka 20 amesema kuwashirikisha viongozi wenzake ndiko kulimwezesha kumudu changamoto alipokuwa Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma aliyoitaja kuwa miongoni mwa maeneo yaliyompa changamoto kwenye utumishi wake.

Nyembo aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya mwaka 1998, wakati huo akiwa katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) mkoani Manyara.

Akitoa nasaha kwa mrithi wake, Tesha aliyetumikia nafasi hiyo kwa miaka sita ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwa kumuamini na kumteua kushika wadhifa huo kwa mara ya kwanza kabla ya kuteuliwa tena na Rais Magufuli alipoingia madarakani.

Kwa upande wake, Dk Masele yeye ametembelea nyayo za Rais Magufuli kwa kuwaasa viongozi na watendaji serikalini kuwa karibu na wenzao wa CCM ili kurahisisha majukumu yao ikiwemo kutekeleza ilani ya uchaguzi wa chama hicho kinachotawala.

“CCM ndiyo inayounda na kuongoza Serikali. Huwezi  kufanikiwa bila kuwa karibu na viongozi wa chama kwa mashauriano na kutatua kero na matatizo ya wananchi,” amesema Dk Masele aliyestaafu tangu Juni, 2017.

Wakuu wa wilaya walioapishwa katika hafla inayoendelea katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na wilaya zao kwenye mabano ni Dk Philis Nyimbi (Nyamagana), Severline Laika (Ilemela), Philemon Lugumiliza (Magu) na Cornel Magembe wa Ukerewe.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz