Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakuu wa mikoa, wilaya wakumbushwa walemavu

873b3a6f883dee4b3d65d67132789ca4.jpeg Wakuu wa mikoa, wilaya wakumbushwa walemavu

Wed, 3 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKUU wa mikoa na wakuu wa wilaya wametakiwa kuweka ajenda za masuala ya watu wenye ulemavu kwenye mabaraza ya mashauriano ya mkoa na wilaya ili waweze kupata huduma bora, haki na ustawi katika jamii zinazowazunguka.

Wito huo ulitolewa juzi na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga alipokutana na kuzungumza na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Tabora pamoja na viongozi wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu (Shivyawata).

Alisema masuala ya watu wenye ulemavu yakijumuishwa kwenye mabaraza ya mashauriano ya mkoa na wilaya itasaidia kuibua mikakati ya ujumuishaji, usimamizi na utekelezaji wa masuala yanayowahusu.

"Katika kuhakikisha mipango ya watu wenye ulemavu inapatiwa ufumbuzi ni bora wakati wa vikao vya mabaraza ya mashaurianao vya mkoa na wilaya mkajumuisha masuala ya kundi hilo maalumu, kwa kufanya hivyo itawawezesha kutambua mahitaji yao ya msingi na hamtawaacha nyuma watu wenye ulemavu katika masuala ya maendeleo," alisema.

Ummy pia alishauri bajeti zinapoandaliwa kuanzia ngazi ya mkoa zijumuishe masuala ya watu wenye ulemavu ili kuhakikisha mipango ya maendeleo ya kundi hilo yanatiliwa mkazo na kuinua kiwango cha utoaji huduma kwa kundi hilo.

“Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli inawajali watu wenye ulemavu sambamba na kuboresha huduma zao za msingi ikiwamo afya, elimu na miundombinu,” alisema.

Naibu Waziri huyo alihimiza kuimarishwa kwa huduma za afya na zenye staha kwa watu wenye ulemavu ikiwamo upatikanaji wa mafuta kwa wenye ulemavu wa ngozi (albino), kuimarisha ulinzi wao, kuwawezesha kiuchumi, kuwapatia elimu jumuishi, kujengewa miundombinu rafiki na kuendelea kutoa elimu kwa jamii nzima kuhusu masuala ya wenye ulemavu.

Aliwataka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuwa walezi wa watu wenye ulemavu waliopo kwenye maeneo yaokwa kujenga ushirikiano na kuwawezesha kujadili mambo yanayowahusu.

Pia aliyataka mabaraza ya watu wenye ulemavu kuwa hai ili wakati wote ili yaweze kujadili namna bora ya kuhudumia kundi hilo.

Aidha, alitumia fursa hiyo kukemea vitendo vya usafirishaji na utumikishaji watu wenye ulemavu kuombaomba mitaani na badala yake amewasihi watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na halmashauri ya asilimia mbili ili waanzishe miradi ya kiuchumi.

"Nitumie fursa hii kuwaomba viongozi wa mikoa kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu watu wenye ulemavu waliopo kwenye maeneo yao kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, halmashauri, kata hadi vijijini ili kuzuia vitendo vya usafirishaji na utumikishwaji watu wenye ulemavu kuombaomba mitaani," alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Philemon Sengati alisema mkoa huo umekuwa mstari wa mbele katika kuhudumia watu wenye ulemavu na kutoa mfano namna uongozi wa mkoa huo umekuwa ukishirikiana na viongozi kwa watu wenye ulemavu katika kushughulikia masuala mbalimbali ya kundi hilo.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Watu wenye Ulemavu, Jacob Mwinula alisema Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kushughulikia na kutatua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu nchini sambamba na kuhakikisha kundi hilo linapata huduma bora.

Chanzo: habarileo.co.tz