Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakuu wa mikoa waonya vitambulisho vya JPM

32556 Vitambulisho+pic Tanzania Web Photo

Thu, 20 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tabora/Mwanza. Wakuu wa mikoa ya Tabora na Mwanza wamegawa vitambulisho vya wafanyabiashara ndogo kwa wakuu wa wilaya huku wakionya kuwa visitumiwe vibaya.

Jana, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri aliwaambia wafanyabiashara hao kuwa watakaovitumia vibaya wajiandae kula sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya wakiwa mahabusu.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vitambulisho hivyo kwa wakuu wa wilaya, mkuu huyo wa mkoa alisema hata wafanyabiashara wakubwa watakaodanganya nao hawatakuwa salama na kuwataka kuwa waaminifu ili asiwepo atakayepata matatizo.

Alisema uongozi wa mkoa haupaswi kulaumiwa kuhusiana na mgawo wa vitambulisho hivyo, ndiyo maana amevigawa sawa kwa halmashauri zote nane huku kila moja ikipata 3,125 bila kujali ukubwa au idadi ya watu.

Mwanasheria wa ofisi ya mkuu wa mkoa huo, Richard Lugomela aliwashauri wakuu wa wilaya kutovigawa pasipo kufuata utaratibu ambao unataka wawatambue kwanza wahusika kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato (TRA).

Akikabidhi vitambulisho kwa wakuu wa wilaya, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema wapo baadhi ya wafanyabiashara wakubwa ambao wameandaa makundi ya vijana ili wachukue vitambulisho na kuwaonywa wasithubutu kufanya hivyo.

“Tumeshapata taarifa kwamba wapo baadhi ya wafanyabiashara wameshawakusanya vijana wao ili wachukue vitambulisho hivi wawe wanawapa bidhaa zao wapange barabarani lengo ni kukwepa kodi,” alisema Mongella.

Aliwataka wamachinga kuacha kutumika kwa madai kuwa kitendo hicho kitavuruga kile alichokiita nia njema ya Serikali ya kuwakomboa.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu akikabidhi vitambulisho kwa wajasiriamali 336 katika mji wa Mugumu, alisema watakaobainika kuvitumia vibaya watanyang’anywa. Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Juma Hamsini alisema kwa kushirikiana na maofisa wa TRA waliandaa mpango wa kuwabaini walengwa ingawa wengi waliojitokeza walibainika kutokuwa na sifa zilizoelezwa na Rais.

Imeandaliwa na Robert Kakwesi, Beldina Nyakeke, Jesse Mikofu na Anthony Mayunga.



Chanzo: mwananchi.co.tz