Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakurugenzi watakiwa kuharakisha ufungaji Luku za maji

Babu 780x470 Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu

Sat, 6 Apr 2024 Chanzo: Mwananchi

Wakurugenzi watendaji wa mamlaka za maji nchini, wametakiwa kuharakisha ufungaji wa mita za maji za malipo ya kabla (Luku) ili kuondoa malalamiko ya bili kubwa na malimbikizo ya madeni.

Agizo hilo limetolewa jana Ijumaa Aprili 5, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu wakati akifungua kikao kazi cha wakurugenzi watendaji wa mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira Tanzania bara, wilayani Hai.

Babu amesema kumekuwepo na malalamiko ya wananchi kupewa bili kubwa za maji na ili kumaliza kilio hicho, ni lazima mamlaka za maji nchini ziharakishe mpango wa ufungaji wa mita za maji za malipo ya kabla.

"Bili za maji zimekuwa na changamoto, wananchi wanalalamikia kupewa bili kubwa za maji na jana wakati Rais akizungumza kwenye hafla ya kuwaapisha viongozi, alisema kumekuwa na malalamiko ya wananchi kuhusu bili za maji, sasa tendeni haki na mtu akalipe bili kulingana na maji aliyotumia.

"Zipo mita zile za malipo ya kabla kama Luku za Tanesco, ugomvi utakwisha kama wananchi wote watafungiwa mita hizi, maana wananchi watatumia kile walicholipia,” amesema.

Babu amewataka wakurugenzi hao, kuheshimu na kutunza rasilimali watu na kuhakikisha wanajenga uhusiano mzuri katika utendaji kazi, ili kuondoa malalamiko na manung'uniko miongoni mwao na kuchochea ufanisi wa kazi.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira wa Wizara ya Maji, Charles Mafie amesema tayari wameanza kufunga mita hizo kwa baadhi ya mamlaka nchini ikiwamo Mamlaka ya Maji ya Iringa na Moshi, hatua inayosaidia kurahisisha ukusanyaji wa maduhuli kwa mamlaka hizo.

"Tumepokea maelekezo ya kuanza kutumia mita za maji za malipo ya kabla, hili tumeshalianza kwa baadhi ya mamlaka na mamlaka nyingine tulianza kufunga kwa taasisi kubwa, bado tunaendelea nalo na linatusaidi katika ukusanyaji wa mapato, kwa kuwa mtu anatumia kadri alivyolipia," amesema.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi, (Muwsa), Kija Limbe amesema maelekezo ya kuwafungia wateja mita za maji za malipo ya kabla wameanza kuyatekeleza na tayari wameshafunga mita hizo kwa wateja 400.

"Sisi Moshi tulishaanza kufunga mita hizi na hii itaondoa changamoto ya wateja kuwa na madeni makubwa. Mpaka sasa tumeshawafungia wateja 400 na zoezi hili linaendelea vizuri.

“Mwitikio wa wananchi ni mkubwa kwa kuwa wengi wanahitaji kufungiwa mita hizi na kwa mwaka huu wa fedha tumepanga kufikia wateja 4,000," amesema Limbe.

Chanzo: Mwananchi