Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakurugenzi wa halmashauri Dar wapanguliwa

11777 WAKURUGENZI+PIC TanzaniaWeb

Tue, 14 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amefanya mabadiliko na uteuzi wa mkuu wa wilaya mmoja na wakurugenzi 41 wa halmashauri za wilaya, miji na majiji.

Katika mabadiliko yaliyotangazwa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Mkoa wa Dar es Salaam umebadilishiwa wakurugenzi wa halmashauri za manispaa nne za Temeke, Ilala, Kigamboni na Ubungo.

Halmashauri ambazo hazijaguswa katika mabadiliko hayo ni Manispaa ya Kinondoni na Jiji la Dar es Salaam.

Katika mabadiliko hayo, aliyewahi kuwa mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Kinondoni, Mussa Natty ameteuliwa tena katika nafasi hiyo kituo chake cha kazi kikiwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduma.

Wateule wapya mkoani Dar es Salaam ni Lusubilo Mwakabibi (Temeke), Beatrice Kwai (Ubungo), Jumanne Shauri (Ilala) na Ng’wilabuzu Ludigija (Kigamboni).

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aaron Kagurumjuli na Mkurugenzi wa Jiji, Siporah Liana wanaendelea na majukumu katika nafasi zao.

Aidha, mabadiliko hayo mkoani Dar es Salaam yamekuja wiki moja baada Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika kufanya uteuzi wa makatibu tawala wa wilaya 18 kujaza nafasi zilizokuwa wazi na kuwahamisha wawili.

Katika mabadiliko hayo, ya makatibu tawala wa wilaya ya yaliyofanywa Agosti 5, Hashim Komba aliyekuwa Temeke alihamishiwa Wilaya ya Iringa na Edward Mpogolo wa Ilala alipelekwa Wilaya ya Dodoma. Nafasi ya DAS wa Kinondoni iliyokuwa wazi ilijazwa na Stella Msoffe.

Mabadiliko yaliyotangazwa jana ni ya tatu kwa wakurugenzi wa halmashauri.

Julai 7, 2016, Rais Magufuli alifanya mabadiliko ya kwanza ya wakurugenzi kwa kuteua wa majiji matano, manispaa 21, miji 22 na wilaya 137 za Tanzania Bara. Kati ya wakurugenzi 185 walioteuliwa, 120 walikuwa ni wapya na wengine 65 walikuwa wa zamani.

Mabadiliko ya pili ya wakurugenzi yalifanyika Septemba 10, 2016 na Rais Magufuli alifanya uteuzi wa wakurugenzi wa halmashauri za wilaya 11, mkurugenzi mmoja wa halmashauri ya mji na mkurugenzi mmoja pia wa halmashauri ya manispaa.

Aidha jana, Dk Kijazi pia alitangaza uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Senyi Ngaga ambaye amechukua nafasi ya Simeon Msafiri aliyehamishiwa wilaya ya Chato.

Alisema wakurugenzi ambao katika mabadiliko hayo wamebadilishiwa vituo vya kazi wanapaswa kwenda kuripoti katika vituo vyao vipya mara moja na ambao wameteuliwa kwa mara ya kwanza, watatakiwa kuripoti kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) jijini Dodoma kesho kwa ajili ya kupata maelekezo kuhusu majukumu yao na kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma.

Pia, Balozi Kijazi alisema wakurugenzi wateule wanaokwenda Tamisemi wanapaswa kuwa na vyeti vyao halisi na nakala za vyeti hivyo zilizothibitishwa kisheria vinavyoonyesha matokeo ya kumaliza elimu ya kidato cha nne, kidato cha sita na taaluma zao.

Wakati huohuo, Waziri Mkuchika amemteua Mnkondo Bendera kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Rungwe kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Moses Mashaka ambaye amepangiwa kazi nyingine.

Bendera anatakiwa kuripoti kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora jijini Dodoma kesho akiwa na vyeti vyake halisi vya elimu ya sekondari na taaluma.

Chanzo: mwananchi.co.tz