Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakurugenzi halmashauri mkoa wa Rukwa mtegoni

298dbea57c894d3bd0b534c70552473f.jpeg Wakurugenzi halmashauri mkoa wa Rukwa mtegoni

Fri, 22 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo ametoa siku tatu kwa wakurugenzi wa halmshauri za mkoa huo kujieleza kwa maandishi sababu za kushindwa kutekeleza maagizo ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Maagizo hayo ni yale yaliyotolewa na Makamu wa Rais mwaka 2015 ya kuzitaka halmashauri nchini kupanda miti isiyopungua milioni 1.5 kila mwaka ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Akitoa agizo hilo mjini hapa jana, Wangabo alisema kwa kipindi cha mwaka 2018/2019 halmashauri nne za mkoa wa Rukwa zilipanda miti milioni 2.5 ambayo ni sawa na asilimia 43, huku mwaka 2019/2020 halmashauri hizo zikipanda miti milioni 1.6 ambayo ni sawa na asilimia 26 ikionesha kushuka katika utekelezaji wa agizo hilo.

“Hali hii haikubaliki, nawaagiza wakurugenzi hao kutoa taarifa ya maandishi kueleza sababu za kushindwa kutekeleza agizo hilo.”

"Tangu Mwaka 2015 hali ya upandaji miti inashuka chini sasa tupo kwenye asilimia 26 ya miti milioni sita, tumepanda milioni 1.6 kwa mkoa mzima wakati uharibifu wa mazingira ni mkubwa, uharibifu wa ukataji wa miti ni mkubwa, shughuli za mifugo, shughuli za ujenzi, mkaa, miti zinaangamiza mazingira lakini hatupandi miti inayolingana na tunayoikata," alisema.

Mkuu huyo wa mkoa aliagiza taarifa hiyo iambatane na mpango kazi wa wakurugenzi hao unaoonesha jinsi walivyojipanga kwa utekelezaji wa agizo hilo kuanzia Januari hadi Aprili mwaka huu.

Aidha, Wangabo aliwataka wakuu wa wilaya za mkoa huo kufanya ukaguzi katika halmashauri zao ili kuhakikisha kila halmashauri imepanda miti milioni 1.5 na inasimamiwa.

"Mimi mwenyewe nimeonesha njia hapa leo (jana) tumepanda miti zaidi ya 100, sasa kinashindikana kitu gani, wenyeviti wa vitongoji wapo, wenyeviti wa vijiji wapo, watendaji wa vijiji na kata wapo, tarafa wapo, maofisa ugani wote wapo, taasisi za shule zipo chungu nzima, hizi tu peke yake ukizisimamia zikapanda miti mingi, lakini juu ya yote kuna wadau mbalimbali wa mazingira tunao hapa," alisema.

Wangabo hayo wakati wa kilele cha siku ya upandaji miti kimkoa inayofanyika Januari 19 kila mwaka, huku akizindua rasmi upandaji miti ya matunda hasa miparachichi katika Gereza la Mollo na kijiji cha Malonje kwa ajili ya kuimarisha vipato vya gereza na wananchi kuwa na zao mbadala la kilimo cha biashara.

Akitoa taarifa fupi ya upandaji wa miti katika Gereza la Mollo Manispaa ya Sumbawanga, Mkuu wa gereza hilo, Englibert Chingalo alisema gereza hilo lilipokea miche 655 kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa hadi kufikia Januari 14 mwaka huu.

"Tangu Gereza la Mollo lianzishwe mwaka 1967 haijawahi kupandwa bustani ya miche ya matunda kama inavyofanyika sasa” alisema.

Kwa upande wake, Meneja wa Msitu wa Mbizi, mkoani Rukwa, Mohamed Kiangi alimuomba mkuu huyo wa mkoa kuboresha programu hiyo aliyoianzisha kwa kuhakikisha inakuwa na usimamizi bora wa miti inayopandwa na takwimu za wapandao hasa miparachichi na halmashauri zichangie gharama za uzalishaji wa miche.

Alisema mti mmoja wa parachchi unakadiriwa kuzalisha matunda 500 huku bei ya tunda moja ikiwa ni Sh 500, hivyo miparachichi 100 iliyopandwa katika Shule ya Msingi Malonje inakadiriwa itazalisha matunda 50,000 ambayo thamani yake ni Sh milioni 25.

Chanzo: habarileo.co.tz