Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakurugenzi Halmashauri nne tumbo joto Arusha

Arusha Pichnjm Wakurugenzi Halmashauri nne tumbo joto Arusha

Tue, 2 May 2023 Chanzo: mwanachidigital

Watumishi wa Serikali wamezishtaki halmashauri nne za Mkoa wa Arusha kuhusu kukiuka muongozo na haki za wafanyakazi katika malipo ya mishahara.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) Mkoa wa Arusha, Lotha Laizer ameyasema hayo jana Mei 1, 2023, katika maadhimisho ya sherehe za Mei Mosi mbele ya mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela kwenye Viwanja vya Sheik Amri Abeid.

Lotha amesema ipo changamoto kubwa kwa wafanyakazi wanaolipwa na Halmashauri kupitia mapato ya ndani kwani mishahara yao inachelewa zaidi ya miezi sita haki inayowanyima kupata huduma muhimu ikiwemo za afya.

"Halmashauri sugu kuchelewesha mishahara ya wafanyakazi ni Karatu, Longido na Arusha jiji tunaomba useme nao, sambamba na Halmashauri ya Ngorongoro ambao wao wamekiuka utaratibu wa kulipa zawadi za wafanyakazi bora, ambapo waliowataja mwaka jana hadi sasa hawajalipwa," amesema.

Lotha amemuomba Mkuu wa Mkoa kufuatilia kwa ukaribu baadhi ya sekta binafsi zinazokiuka muongozo wa Serikali wa kima cha chini cha mishahara,

“Hadi leo bado kuna taasisi zinalipa kipato kidogo ambacho hakiendani na mfumo wa maisha wa sasa hasa mfumuko wa bei za huduma na bidhaa mbalimbali kama chakula mbali na hilo baadhi ya waajiri hawataki kufungua tawi la wafanyakazi katika maeneo yao jambo ambalo ni kinyume na sheria na taratibu hasa wafanyakazi wanapokumbwa na changamoto wanakosa pa kupeleka matatizo yao," amesema.

Akijibu hoja hizo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela ameziagiza Halmashauri za Longido, Karatu na Arusha jiji kulipa mishahara yote ya wafanyakazi wanaodai ndani ya wiki moja kuanzia siku ya leo Jumatatu.

"Mapato yanapokuwa wao ndio wamefanya kazi sasa haiwezekani msiwalipe, naagiza wakurugenzi wa hizi Halmashauri watendeeni haki wafanyakazi hawa, lakini halmashauri ya Ngorongoro acheni utani na haki za watu nataka ifikapo Ijumaa wiki hii nipate uthibitisho wa wale wafanyakazi bora kupewa zawadi zao," amesema.

Awali akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Katibu wa Tucta Mkoa huo, Abrahamu Kamwela aliwasilisha maombi yao saba mbele ya Mongela ikiwemo kuongezewa mishahara kuendana na ongezeko la bidhaa sokoni, kupunguziwa makato ya kodi ili waweze kupambana na uchumi.

"Mkuu wa mkoa, tunaomba Rais Samia pia atuboreshee huduma za afya lakini pia idhibiti sekta biafsi iendelee kuwapatia bima za afya wastaafu wao kama walivyo wengine wa serikalini, lakini pia tunaomba tume iongeze ofisi kila kanda ili kuharakisha maamuzi ya rufaa za watumishi," alisema.

Chanzo: mwanachidigital