Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima wa mkonge walilia uhaba wa wataalamu na soko

61023 Mkonge+pic

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Morogoro. Wakulima na wazalishaji wa nyuzi za mkonge mkoani Morogoro wameiomba Serikali kufufua kituo cha kufundishia wataalamu wa zao hilo kilichopo Mlingano Jijini Tanga kwa kuwa hivi sasa hakuna wataalamu wa kutosha.

Ombi hilo limetolewa Juni mosi mwaka 2019 na Mkurugenzi wa kampuni ya Highland Estates Limited inayomiliki shamba la mkonge la Pangawe Estates, Naweed Mulla wakati Naibu waziri wa Kilimo Omary Mgumba alipofanya ziara katika shamba hilo.

Mulla ambaye kampuni yake pia ina kiwanda cha kutengeneza nyuzi za mkonge amesema wataalamu wanaohitajika katika sekta ya mkonge ni pamoja na wataalamu wa mashambani, wataalamu wa kuendesha mashine za kutengeneza nyuzi (kolona) pamoja na wataalamu wa kutengeneza vipuri vya mashine hizo.

Amesema tangu kampuni hiyo ikabidhiwe shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 3600 mwaka 2007, kumekuwa na changamoto ya wananchi kuvamia baadhi ya maeneo ya shamba hilo na kufanya kilimo jambo ambalo linazua mgogoro ambayo mpaka sasa kampuni inashirikiana na Serikali kuitatua.

Meneja uzalishaji na ushauri wa shamba la mkonge la Fatemi Estate linalomikiliwa na kampuni ya Mohamed Enterprisess Tanzania Limited (MeTL) lililopo kata ya Kidugalo Wilaya ya Morogoro Ndekilwa Nyari ameiomba Serikali kuongeza matumizi ya magunia katika kuhifadhi nafaka mbalimbali ili zao la mkonge liweze kupata soko.

Nyari ametaja changamoto ya uingizaji mifugo kwenye mashamba ya mkonge kuwakuwa unasababisha uharibifu hasa kwa mkonge mchanga hivyo aliiomba Serikali za vijiji na Halmashauri kuweka sheria kali ili kudhibiti wafugaji wanaoingiza mifugo katika shamba hilo.

Pia Soma

Katika tukio hilo Mkurugenzi wa bodi ya mkonge nchini Yunusi Musika amesema wananchi wengi bado hawajahamasika kulima zao la mkonge hivyo lazima ziwekwe juhudi za makusudi za kuinua na kuendeleza zao hilo ambalo kwa sasa ni zao pekee lisiloathirika na mabadiliko ya tabia nchi.

“Kwa sasa Tanzania inashika nafasi pili duniani kwa uzalishaji wa mkonge huku nchi ya Brazil ikishika nafasi ya kwanza, Mkonge unaozalishwa hapa nchini una ubora kuliko hivyo kama tutaweka mkazo kwenye zao hili tutaweza kupata masoko ya uhakika popote duniani,” amesema Musika.

Naibu Waziri Mgumba amesema Serikali  itaendelea kuhakikisha mazao yote ya kimkakati yanasimamiwa kwa karibu kuanzia kwenye utafiti, uzalishaji, uchakataji na hata kwenye kupata masoko.

Chanzo: mwananchi.co.tz