Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima wa korosho Hai wafundwa

C147521e506804b5c2ace99c9337311c Wakulima wa korosho Hai wafundwa

Mon, 30 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BODI ya Korosho Tanzania (CBT) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imetoa mafunzo kwa wakulima na maofisa kilimo wilayani Hai kuhusu kilimo bora cha zao la korosho na ubora wake.

Mafunzo hayo ya siku mbili yalifanyika wilayani humo hivi karibuni ambapo wakulima wa zao hilo walisema watajitahadi kuhakikisha kilimo cha korosho kinaleta tija kwa kuwa ni zao la kimkakati litakalokuza uchumi wa wakulima na halmashauri.

Mkulima Ester Mbatian kutoka Bomang'ombe alisema mafunzo yatawasaidia kujikita kwenye kilimo cha kisasa kwa kupanda mbegu bora zitakazowapatia mazao ya kutosha ya korosho.

"Wakati naanza kupanda miche ya mikorosho shambani kwangu sikuwa na elimu ya kutosha kuhusu kilimo bora cha zao hili, lakini kupitia mafunzo yaliyotolewa na wataalamu wetu, yatanisaidia mimi binafsi pamoja na wakulima wenzangu kuboresha kilimo hiki kwa kulima kitaalamu kwa kufuata kanuni za kilimo bora cha korosho," alisema Mbatian.

Mkulima mwingine, Glory Makawaia, alisema elimu waliyopewa imewasaidia kujua mbegu bora na matumizi sahihi ya dawa ya kudhibiti wadudu na magonjwa katika mikorosho.

Ofisa Kilimo wilayani humo, David Lekei aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia elimu iyotolewa na wataalamu kwasababu wanawakilisha kundi kubwa wakiwemo wakulima pamoja na wataalamu katika zao hilo kwenye maeneo husika.

Wataalamu kutoka Tari Naliendele akiwemo Ofisa Uhaulishaji Teknolojia na Mahusiano wa Tari Naliendele, Stella Andrea, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwapatia wakulima teknolojia mpya za kilimo bora cha zao la korosho kwa kupanda mbegu bora na kudhibiti wadudu waharibifu na magonjwa katika zao hilo.

Mtafiti upande wa wadudu waharibifu na magonjwa ya korosho, Dadili Majune wa Tari, alisema kuna magonjwa ya mikorosho zaidi ya 12 yanayofahamika kushambulia mikorosho hapa nchini ukiwemo Ubwiri Unga, Blaiti ya mikorosho, Unyaufu wa mikorosho pamoja na Debeki.

Chanzo: habarileo.co.tz