Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakulima kukopeshwa mabilioni kwa riba nafuu

Mkulima Ed Wakulima kukopeshwa mabilioni kwa riba nafuu

Fri, 5 Nov 2021 Chanzo: ippmedia.com

WAKULIMA wadogo wametangaziwa neema, baada ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuingia katika makubaliano na Maendeleo Benki kuwawezesha kupata mikopo yenye riba nafuu.

Lengo ni kuwawezesha kuongeza uzalishaji na kufanya mageuzi katika sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji.

Makubaliano hayo, yaliyosainiwa katika makao makuu ya TADB jijini Dar es Salaam, yataiwezesha benki hiyo kutoa dhamana ya Sh. bilioni mbili kwa wakulima watakaokwenda kuomba mikopo Maendeleo Benki kufanya shughuli za kilimo, ufugaji pamoja na uvuvi kwa riba nafuu ya asilimia isiyozidi 15. Dhamana hii inaratibiwa na TADB chini ya mfuko maalum wa dhamana kwa wakulima wadogo nchini ‘SCGS’. 

“TADB inaendeleza dhamira yake ya kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wakulima wadogo na wa kati. Wakulima wetu nchini wanapata changamoto ya mitaji. Wengi wakilazimika kukopa kwa riba za kibiashara ambapo wengi wao wamekuwa wakipata changamoto ya kuhimili riba hizo kubwa. Hivyo, kama taasisi ya maendeleo ya kifedha, kupitia mfuko wa dhamana kwa wakulima wadogo, tumeona umuhimu wa kutoa mikopo hii nafuu kwa kushirikiana na Maendeleo Bank ili kuwawezesha wakulima wengi zaidi kupata mitaji,” alieleza Derick Lugemala, Mkurugenzi wa TADB.

Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha biashara wa Benki ya Maendeleo, Emmanuel Mwaya, alisema mikopo hiyo watakayokuwa wanatoa kwa dhamana ya TADB itawawezesha kuwakopesha wakulima wadogo mikopo ya mtaji hadi kiwango cha Sh. milioni 50 kwa mkulima mmoja mmoja, Sh. Milioni 500 milioni kwa vikundi na vyama vya wakulima, na hadi Sh.bilioni 1 kwa kampuni ambazo miradi yake inawaunganisha na kuwanufaisha wakulima wadogo wengi.

 “Ili kupata mikopo hii, mkulima anahitaji kufika katika tawi letu lolote kwa kuwa mikopo hii inapatikana katika matawi yetu yote. Tunatoa rai kwa wakulima wote wadogo kuchangamkia fursa hii.”

Awali, Lugemala alisema lengo la mikopo hiyo yenye masharti nafuu ni kuchagiza benki za kibiashara na taasisi za kifedha kutoa mikopo zaidi kwa wakulima na kuwezesha ukuaji wa minyororo yote ya thamani yanayohusiana na kilimo, uvuvi na ufugaji nchini.

“Mpaka Desemba 2020, mfuko huu wa dhamana ulikwisha toa mikopo katika miradi ya kilimo, uvuvi na ufugaji yenye thamani ya Sh. bilioni 106 na kuwafikia wanufaikaji zaidi ya 11,000 moja kwa moja na wasionufaika moja kwa moja 750,000. Baadhi ya miradi tuliyowezesha ni pamoja na mnyororo wa thamani wa mazao ya korosho, mpunga, kahawa, miwa, mahindi, mihogo, pamba na ufugaji wa kuku,” alifafanua Lugemala.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka TADB, mfuko huu wa dhamana ulianzishwa Februari 2018. Na katika kipindi cha miaka mitatu sasa, TADB imeshashirikiana na benki na taasisi za kifedha kama NMB, CRDB, Azania, Benki ya Posta (TPB), Stanbic, FINCA Microfinance, UCHUMI Commercial Bank, Tandahimba Community Bank (TACOBA), Mufindi Community Bank (MUCOBA), NBC na Maendeleo Bank.

“TADB inaamini kwamba kupitia mtandao huu wa ushirikiano wa kimkakati, idadi kubwa ya wakulima wadogo watafikiwa na kuwezeshwa,” alisisitiza Lugemala.

Chanzo: ippmedia.com