Siku chache baada ya baadhi ya Wakulima wa Vijiji vya Mwitikira, Ndaleta, Katikati na Ngabolo Wilayani Kiteto Mkoani Manyara wanaodai kuporwa maeneo yao ya mashamba kuamua kurejea katika mashamba hayo, baadhi yao wamekamatwa na kushikiliwa na Jeshi la Polisi wakidaiwa kuvamia sehemu ya Hifadhi.
Wakulima hao waliandaa jumbe mbalimbali kuelekeza kwa viongozi wa Serikalini akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na Chama cha Mapinduzi wakiwaomba kuingilia mgogoro huo kwa madai kuwa wameporwa ardhi na Wafugaji ambao wanatumia maeneo hayo kulisha mifugo huku wakilindwa na baadhi ya viongozi wa Wilaya na Mkoa.
Akizungumzia mgogoro huo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara, George Katabazi anasema: “Kuna wakulima 27 tunawashikilia kutokana na kuingia katika maeneo ya Hifadhi ya Wanyama ya Makame inayosimamiwa na WMA.
“Askari wa Hifadhi walienda kuwaondoa lakini wakakuta wahusika wana silaha za jadi ikabidi waombe msaada kutoka Jeshi la Polisi ndipo tukafanikiwa kuwashikilia.
“Sehemu hizo kuna migogoro ya muda mrefu ya masuala ya ardhi, imetokea wakati huu kwa kuwa ni kpindi cha kuandaa mashamba, kila mwaka ikifika wakati wa kilimo migogoro inaanza.
“Kukiwa na jinai watafikishwa Mahakamani, mara nyingi Polisi wanapofanya utekelezaji wa kazi za Kijamii wanaonekana wabaya, tusipoingilia kungeweza kutokea jambo baya kati ya Wakulima na Afisa wa WMA.
“Kitakachofanyika tutawaomba nyaraka zao (Wakulima) ili kuona kama wana hati au vibali vya kulima maeneo hayo au kama hawana, kama wanazo basi hatua nyingine zitafuata.
“Kuna changamoto kubwa ya migogoro ya aina hiyo na nadhani elimu zaidi inatakiwa kutolewa kwa kuwa WMA nao wana maeneo yao ambayo hayana uhusiano na hifadhi.
“Wakulima kama wakiwa na hoja ya kuongezewa maeneo kwa ajili ya kulima.”
Kuhusu hoja kuwa kuna Wafugaji wanaotumia maeneo hayo ya hifadhi kwa ajili ya mifugo na ndio maana Wakulima nao wanaona jambo hilo si sawa, Kamanda anafafanua:
“Hifadhi za WMA kuna maeneo ambayo yamehifadhiwa kwa ajili ya Wanyama, ni jamii yenyewe ndio wanakubaliana na Serikali ya Kijiji pamoja na WMA kama kuna maeneo kuwe na malisho au iwe ni kwa ajili ya Wanyama, hivyo ni suala linalozungumzika.
“Mara nyingi uzoefu unaonekana ufugaji na kilimo vyote vinaweza kuathiri hifadhi lakini kulisha mifugo mara nyingi inakuwa na athari zaidi kuliko kuwa na kilimo.”