Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakubaliana kusimamia kwa pamoja maji Bonde Mto Rufiji

98b3c728b06e0960926ee1c183a558ef Wakubaliana kusimamia kwa pamoja maji Bonde Mto Rufiji

Mon, 23 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WADAU sekta mtambuka wa Bonde la Mto Rufiji wameazimia kutekeleza mpango wa pamoja wa usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji katika bonde hilo ili kuweka mizania ya matumizi ya maji shindani, hatua itakayozinufaisha sekta zote zinazotumia rasilimali hiyo.

Mkurugenzi wa Bodi ya Bonde la Mto Rufiji, Florence Mahay alisema hatua hiyo itachochea ushirikiano na matokeo endelevu katika usimamizi wa rasilimali za maji na mgawanyo wa maji kwa kuzingatia mahitaji ya kila sekta.

Azimio la mpango huo lilifikiwa mjini Iringa juzi katika jukwaa la siku mbili la wadau wa sekta hiyo.

Mahay alisema utekelezaji wa mpango huo utakwenda sambamba na kuvitambua vyanzo vyote vya maji katika bonde hilo ili kuvihifadhi na kuvilinda pamoja na kuwatambua watumiaji wake wote wa maji ya bonde hilo, wenye vibali na wasio na vibali.

Pamoja na kwamba zaidi ya asilimia 70 ya maji ya bonde hilo yanaenda kwenye sekta ya kilimo, Mshauri wa Bodi ya Bonde hilo la Rufiji, Patrick Valenda alisema: "Inakadiriwa asilimia 30 tu ya maji hayo ndiyo yanayotumika kwa shughuli hiyo huku nyingine 70 zikipotea."

Valenda alisema ili kukabiliana na changamoto ya kuongezeka kwa mahitaji ya maji kutokana na ongezeko la watu na ukuaji wa shughuli zao za kimaendeleo huku tafiti zikionesha kiwango chake duniani kinazidi kupungua; maamuzi mazuri lazima yafanywe kwa pamoja kuzidisha matokeo yanayohitajika na kupunguza yasiyotakiwa, hatua itakayoleta matokeo endelevu katika utoaji wa huduma zilizokusudiwa na kuondoa migogoro.

Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Maji, Rosemary Rwebugisa alisema Sera ya Maji ya Taifa ya Mwaka 2002 imeweka utaratibu wa haki ya kuyafikia maji na ugawaji wa rasilimali za maji ili sekta zote za kijamii na kiuchumi ziweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Mmoja wa washiriki wa jukwaa hilo, Julius Mwanibingo kutoka jumuiya ya watumiaji maji wa bonde dogo la mto Mkoji alisema ili sekta hiyo isiathirike ni lazima nguvu ya kuhifadhi na kuvilinda vyanzo vya maji iwe sawa au zaidi ya ile inayotumika katika ugawaji wa maji.

Naye Mhifadhi Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Sharif Abdul alisema mpango wa pamoja wa usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji katika bonde hilo ulioridhiwa na wadau unatarajiwa kurejesha mtiririko wa maji kwa mwaka mzima katika mto Ruaha Mkuu unaopita hifadhini humo.

Chanzo: habarileo.co.tz