Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakina baba hebu msikieni RC huyu

55704 BABA+P

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Simiyu. Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amewataka akina baba kuwasindikiza wake zao kliniki wakati wa ujauzito ili kuhakikisha wanapatiwa chanjo zote muhimu kwa ajili ya kumlinda mama na mtoto na magonjwa mbalimbali ikiwamo pepopunda.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ iliyofanyika mkoani kwake mwishoni mwa wiki, Mtaka alisema kila mtu ana wajibu wa kuhakikisha mama mjamzito na mtoto atakayemzaa wanakuwa salama kiafya ba kutopoteza uhai.

“Ni wajibu wa kila mtu, kuanzia ngazi ya familia kuhakikisha mama mjamzito anakwenda hospitali na siyo kujifungulia nyumbani,” alisema.

Mtaka alisema Serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa kujenga hospitali na zahanati kila sehemu nchini hivyo hakuna sababu ya mama mjamzito kujifungulia nyumbani hata kama hospitali ipo mbali.

‘Elimu ya afya ya uzazi itolewe kwa jamii, wakiwamo wanawake na wasichana, juu ya umuhimu wa kwenda hospitali, kliniki wakati wa ujazito na baada ya kujifungua.”

“Tuna aina nyingi za usafiri katika sehemu nyingi za mazingira yetu, gari, pikipiki na hata baiskeli, hivyo mama mjamzito awahishwe mapema hospitali ili kumlinda na madhara yanayoweza kujitokeza,” alisema Mtaka.

Naye Naibu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Dk Hashina Begun alisema shirika hilo linaungana na Serikali na mashirika mengine kuhakikisha vifo vya mama mjamzito na mtoto mchanga vinapungua.

Miongoni kwa sababu zinazotajwa kusababisha vifo hivyo ni wajawazito kutokwa na damu nyingi wakati na baada ya kujifungua, ukosefu wa chanjo zinazopelekea magonjwa mbalimbali kama pepopunda na kifafa cha mimba.

Kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’, inatekelezwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali, ikiwamo Shirika la Kuhudumu Watoto Duniani (Unicef).



Chanzo: mwananchi.co.tz