Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakemia waaswa kuwa waadilifu

61020 Wakemia+pic

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko, amewasisitiza wakaguzi wa kemikali na maabara za kemia kuzingatia weledi, uadilifu na uaminifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Dk Mafumiko amezungumza hayo leo  Juni 2, 2019 wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Wakaguzi wa Kemikali na Maabara za Kemia kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali unaofanyika katika ukumbi wa Baraza la Maaskofu, Kurasini, jijini hapa.

 “Serikali imetupa majukumu ya kusimamia Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Sheria ya Vina saba vya Binadamu na Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani, hivyo tunapaswa kuzingatia weledi, uadilifu, uaminifu na upendo ili kuhakikisha tunatekeleza majukumu yetu kwa ufanisi," amesema Dk Mafumiko.

Dk Mafumiko amewapongeza watumishi wa ofisi yake kutokana na kazi kubwa wanayofanya kwakuwa inawahamasisha kuboresha zaidi huduma kwa wadau na kufuata Sheria, taratibu na kanuni zinazowaongoza kama watumishi wa umma.

“Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti inatambua mchango mkubwa wa wakaguzi katika kusimamia Sheria na kuingiza maduhuli ambayo taasisi inatumia katika kuboresha huduma na kujiendesha, Tunatambua changamoto kama kuongeza watumishi na vitendea kazi tunaendelea kuzifanyia kazi" amesema.

Amesema kuna maeneo ya msingi ya kuyawekea kipaumbele akiutaja uwekezaji katika mitambo ya kisasa ya maabara na teknolojia ili kuwawezesha wakaguzi kutoa huduma bora na za haraka kwa wadau.

Pia Soma

Amewataka kufanya kazi kama familia ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na mafanikio.

Katika mkutano huo Mkaguzi wa Kemikali, Jovitus Mukela amesema wao ni jukumu lao kutekeleza maelekezo na kutenda kazi zao kwa mujibu wa sheria.

"Tukitoa huduma nzuri tutakuwa tumeitendea haki  Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, wananchi, wadau, sisi  na nchi kwa ujumla" amesema Mukela.

Chanzo: mwananchi.co.tz