Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakazi waiomba Serikali ijenge kivuko kwenye korongo

BVVkvyPw.jpeg Wakazi waiomba Serikali ijenge kivuko kwenye korongo

Thu, 11 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakazi wa Mtaa wa Ihumwa Madukani jijini hapa wameiomba Serikali iwawekee kivuko cha watembea kwa miguu na vyombo vya moto kwenye korongo linalounganisha mtaa huo na Mtaa wa Chilwana.

Hayo yameelezwa leo Januari 11, 2024 na wakazi wa eneo hilo walipozungumza na Mwananchi Digital na kuongeza kuwa, kukosekana kwa kivuko imekuwa adha kwao.

Wamesema wanahatarisha maisha yao wakiwa wanavuka eneo hilo hasa msimu huu wa mvua.

Mkazi wa mtaa huo, Julius Chedego amesema wanachotaka korongo hilo kujengewa ili wapate kivuko cha kuvuka ng’ambo ya pili kwa sababu lisipojengewa litazidi kulika na kusogea kwenye makazi ya watu.

“Sasa wametuletea mkandarasi ambaye anatumia sululu kuchimba mtaro kweli hii inaingia akilini sisi tunataka kivuko cha kudumu,” amesema Julius Chidego

Mkazi mwingine, Emmy Chiwanga amesema kukosekana kwa kivuko ni kilio kikubwa kwa kuwa watoto wamekuwa wakikosa masomo hasa kipindi hiki cha mvua kwa kuhofia kubebwa na maji.

Pia, Patrick Sangoda amesema ukosefu wa kivuko kunawasababishia kupoteza muda wao mwingi kwa kuzunguka umbali mrefu ili kukwepa eneo hilo.

“Hii ni sehemu kubwa inayounganisha ng’ambo na ng’ambo, kwa sisi tunaoamka na kwenda kutafuta riziki zetu mjini, inatugharimu kwa sababu tunatumia si chini ya Sh30,000 kufika makazini kwetu,” amesema Sangoda.

Dereva wa bodaboda, Abuu Yasin ametoa wito wake kwa Serikali kutengeneza eneo hilo korofi kwa kuwa limekuwa likiwatatiza kwenye shughuli zao za kila siku hasa usafirishaji.

Pia, Yasini ameonyesha wasiwasi wake namna korongo hilo linavyoongezeka siku hadi siku.

“Napata wasiwasi juu ya eneo hili kwa kuwa, jinsi siku zinavyozidi korongo linaongezeka na kufuata makazi ya watu,kwa hiyo Serikali iangalie inavyoweza kutusaidia kabla majanga makubwa hayajatokea,” amesema Yasin.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Ihumwa Madukani, William Njilimui amesema ni kweli wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakiteseka kwa kukosa kivuko kwa miaka miwili sasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live