Mtwara. Imeelezwa wakazi wa mji wa Mtwara nchini Tanzania wataendelea kukumbwa na mgao wa huduma ya maji licha ya mradi wa kuhamisha mabomba kupisha ujenzi wa barabara unaotegemewa kukamilika Agosti 30, 2019 kukamilika kwa zaidi ya asilimia 90.
Akizungumza leo Jumatano, Agosti 28, 2019 Kaimu mkurugenzi wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira mjini Mtwara, Sauna Keya amesema kazi za msingi zilizokuwa zinafanyika zimekamilika licha ya kwamba umechukua zaidi ya miezi miwili kama ilivyotegemewa.
“Wananchi watuvumilie kwa siku hizi chache zilizobaki na siku za mwanzo baada ya tarehe 30 kwa sababu bado maji yataendelea kuwa kwa mgao lakini wingi wa maji utaongezeka sio kama ulivyokuwa kwa sasa maji yalipungua kwa sababu ya mabomba yanayotoa maji uwezo wake ulipungua,” amesema Keya
“Maji bado ni ya mgao wananchi wayatunze, mradi huu ulikuwa hauongezi vyanzo vingine vya maji zaidi ya kuhamisha mabomba kupisha ujenzi wa barabara, kwa hiyo maji tuliyokuwa tukiyatoa mwanzo ndio hayohayo tutaendelea kutoa japo siku za mbeleni tutaongeza vyanzo vya maji,” amesema
Meneja wa mradi huo, Ramadhani Chubi amesema kwa sasa wanamalizia kuunga bomba kubwa na kwamba mkandarasi tayari ameshapokea malighafi zilizokuwa zikihitajika.
Meneja biashara, Judithi Namwereni amewataka wananchi ambao hawapati maji hata kwa mgao kutoa taarifa ili kufuatilia mabomba yao kabla ya kukamilika ili kuepuka kuchimbua bomba hilo upya kuwaunganisha.
Pia Soma
- Trump akandia waandishi kuandika 'mafuriko' ya kampeni za mpinzani
- Kikongwe aliyepigania ardhi yake kwa miaka 42 kulipwa milioni 500
- Chama cha wachapishaji Tanzana chataja changamoto tatu zinazokikwamisha