Wakazi wa Kipawa na Tabata jijini Dar es Salaam wameiomba Serikali kuwajengea daraja la Mto Msimbazi litakalowasaidia kuvuka kwenda kufanya shughuli zao.
Kukosekana kwa daraja hilo kunawafanya watumie fedha kuwalipa wavushaji kuanzia Sh1,000 kwa awamu moja.
Wakizungumza leo June 5, 2023 baada ya Mwananchi kutembelea sehemu hiyo wakati mvua inyesha na kushuhudia watu wakibebwa na kuvushwa upande wa pili, baadhi yao walidai hali hiyo imekuwa kawaida kila mvua zinaponyesha.
“Naishi Kipawa ila shughuli zangu za kujiingizia kipato ziko Tabata na ili nifike nilazima nivuke sehemu hii, sasa kila siku natumia Sh2,000 ambapo kwenda Sh 1,000 na kurudi na kiasi hicho,”amesema Habibu Mussa
Ramadhan Mwangobele mmoja wa vijana wanaowavusha wakazi hao, amesema kazi hiyo wanaifanya kama msaada tu ili kuhakikisha mtu asije kupata madhara.
“Tulijitosa kufanya kazi hii baada kuona wengi wanakosa msaada na barabara hii inatumiwa na watu na imeshawahi kutokea watu kusombwa na maji,”amesema Mwangobele
Amesema ni vijana wengi wanaofanya shughuli hiyo na kwamba wamekuwa wakivusha hadi wanafunzi ambao anadai wanatoza Sh500.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Tabata Barakuda, Melito Solly amekiri kuwa na changamoto hiyo kwa muda mrefu huku akieleza wameshakubaliana na kampuni inayozoa mchanga eneo hilo kuwajengea daraja.
“Tumepata mfadhili ambaye ni mtu anayezoa mchanga mto msimbazi katika kusaidia jamii ya hapa ametuahidi kujenga daraja na hata wananchi wangu nimeshawaambia wa mtaa wa Mfaume na Karakata,”amesema