Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakazi Ukara wafurahia ujenzi wa kivuko kipya

19034 Pic+ukara TanzaniaWeb

Mon, 24 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ukara. Wakazi wa kisiwa cha Ukara wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza wameelezea kufurahishwa na uamuzi na hatua zilizochukuliwa na Serikali kuhusiana na tukio la ajali ya Kivuko cha Mv Nyerere kilichopinduka Septemba 20,2018.

Uamuzi iliowafurahisha zaidi wakazi wa kisiwa hicho chenye kata nne zinazokaliwa na watu zaidi ya 150,000 ni kujengwa kwa meli mpya ya tani 50 yenye uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 200 ambayo ni mara mbili ya idadi iliyokuwa ikibebwa na Mv Nyerere.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutangaza uamuzi huo, baadhi ya wakazi wa kisiwa cha Ukara wamesema uamuzi wa kujenga meli mpya umejibu kilio cha muda mrefu cha wananchi wa eneo hilo.

"Wakazi wa kisiwa cha Ukara wanategemea gulio la Bugolora kupata mahitaji muhimu; kwa sababu gulio hilo hufanyika mara moja kwa wiki, idadi ya abiria kutoka na kurudi Ukara siku ya Alhamisi huongezeka maradufu kulinganisha na siku nyingine," amesema Stephen Matui, mkazi wa kijiji cha Bugaramila kilichopo Kisiwa cha Ukara

Anaongeza; "Kupatikana meli mpya na kubwa zaidi itakayofanya safari nyingi zaidi kutapunguza msongamano wa abiria siku za gulio."

Moja ya sababu ya idadi kubwa ya vifo katika ajali ya Mv Nyerere kwa mujibu wa taarifa ya Serikali iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa, Isaac Kamwelwe ni kujaza abiria na mizigo kuliko uwezo wa kivuko.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Kamwelwe ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, miili 225 ya waliokufa tayari imeopolewa huku watu 41 wakiokolewa wakiwa hai.

Kivuko cha Mv Nyerere kina uwezo wa kubeba abiria 101 na magari matatu lakini siku ya tukio inaaminika ilipakia abiria wengi kutokana na takwimu ya waliokufa na waliookolewa hadi sasa kufikia watu 266.

Akizungumzia kutenguliwa kwa bodi ya Temesa na kusimamishwa kwa Mtendaj Mkuu wa taasisi hiyo, Thomas Mgasa, mkazi wa kijiji cha Bwisya amepongeza uamuzi huo na kuiomba Serikali kuchunguza kwa makini kiini cha ajali hiyo na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wote watakaobainika kufanya uzembe uliosababisha ajali.

Neema Mahoja na Dorcas Majuni wameiomba halmashauri ya wilaya ya Ukerewe kuanzisha gulio katika kisiwa cha Ukara ili kuwaondolea wakazi wa eneo hilo adha ya kutegemea gulio la Bugolora kwa mahitaji yao ya kila siku.

"Kisiwa cha Ukara kinastahili kuwa na gulio lake angalau mara moja kwa wiki badala ya kutegemea gulio la Bugorola," amesema Dorcas.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz