Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakazi Tunduru walia kukatika kwa umeme, Tanesco waomba radhi

89347 Umenme+pic Wakazi Tunduru walia kukatika kwa umeme, Tanesco waomba radhi

Fri, 20 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tunduru. Wakazi wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wamelilalamikia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutotoa taarifa za kueleweka licha ya umeme kuwaka na kukatika kwa siku tano mfululizo huku kuanzia juzi  hadi leo Ijumaa Desemba 20, 2019 ukikatika kabisa na kusababisha wawe gizani.

Wamesema hali hiyo imesababisha wafanyabiashara wa vyakula kupata hasara.

Wakizungumza na Mwananchi leo, Aidan Mzava mkazi wa Mlingoti  amesema tangu wiki iliyopita umeme umekuwa tatizo, “tunalazimika kulala gizani na kuamka bila umeme. Hali hii inakwambisha shughuli za biashara. Jana tu nimepata hasara maana samaki wote wameoza.”

Ameutaka uongozi wa Tanesco kujenga utaratibu wa kutoa taarifa kwa wananchi linapotokea tatizo ili waweze wajipange.

Imani Kalembo, meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (Tamcu) amesema wamelala gizani na wakati mwingine kulazimika kutumia jenereta.

“Tumelazimika kutumia pesa nyingi  kununua  mafuta kwa ajili ya kuwasha jenereta kutwa nzima ili kuweza kuendesha shughuli za hapa ofisini. Bila hivyo tungekwama hata kuendesha mnada. Tunaomba  Tanesco watusaidie kutatua tatizo hili mapema,” amesema Kalembo.

Meneja wa Tanesco Wilaya ya Tunduru,  Joseph Mtula ameomba radhi kwa tatizo lililojitokeza  akibainisha kuwa njia ya umeme kutoka Songea ina hitilafu, itatatuliwa mapema.

“Tumegundua TF (njia) imepigwa radi na bush zake zote kusambaratika  hilo tatizo linafanya njia ya umeme kutoka Songea kukatika. Poleni kwa usumbufu uliojitokeza na tunawaomba muendelee kutuvumilia mafundi wetu wapo kazini usiku na mchana ili kurejesha umeme,” amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz