Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakazi Mji Mkongwe waingiwa na hofu

Mon, 23 Apr 2018 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKATI mvua za masika zikiendelea kunyesha nchini kote, baadhi ya wakazi wa Mji Mkongwe wameingiwa na hofu, kufuatia majengo mengi yaliyopo, kuchakaa na kukabiliwa na tishio la kuporomoka.

Ismali Juma, mkazi wa Kiponda eneo la Mji Mkongwe, alisema wanaishi katika maisha ya hofu ya kuangukiwa na nyumba zilizopo jirani, ambazo zimechakaa. Alisema wakazi wengi wamekuwa wakizihama kwa muda mrefu.

Alisema juhudi zinatakiwa kuchukuliwa ili kuzifanyia ukarabati nyumba hizo, ambazo zinatishia maisha ya wakazi jirani na wapita njia.

Alisema kipindi hiki cha mvua za masika, baadhi ya nyumba hizo ambazo zilizojengwa zaidi ya miaka mia moja, haziwezi kustahimili zaidi zikivujiwa na mvua.

“Tunaziomba taasisi husika zinazoshughulikia maendeleo ya Mji Mkongwe kuzifanyia ukarabati nyumba hizi, ambazo ni tishio kwa maisha ya wananchi na wapita njia,” alisema.

Mapema, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mji Mkongwe Zanzibar, Issa Makarani alikiri majengo yaliyopo Mji Mkongwe wa Zanzibar ni chakavu na ni tishio kwa wakazi wake na wageni.

Alisema Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe, inaendelea kuzifanyia ukarabati nyumba hizo hatua kwa hatua, ingawa changamoto kubwa ni fedha.

Akifafanua kuwa nyumba zilizopo Mji Mkongwe, baadhi zinamilikiwa na wananchi binafsi, majengo ya serikali na wakfu na mali ya amana.

Kwa mfano, alisema nyumba zinazomilikiwa na wananchi, changamoto yake kubwa ni uwezo wa wananchi wenyewe kuzifanyia ukarabati nyumba hizo, ikiwemo tatizo la fedha. Majengo mengi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar wakati wa utawala wa Sultani wa Oman.

Chanzo: habarileo.co.tz