Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakazi Makongo Juu walia ubovu wa barabara

80935 Pic+makongo Wakazi Makongo Juu walia ubovu wa barabara

Mon, 21 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakazi na watumiaji barabara inayopita eneo la Makongo Juu wameiomba Serikali ya Tanzania kuingilia kati ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita tano iliyogeuka kero kutokana na kupitika kwa shida.

Ubovu wa barabara hiyo umetajwa kuwa chanzo cha kudorora kwa uchumi, madhara kiafya na  shida ya usafiri hasa kwa wanaotegemea usafiri wa umma, huku wenye usafiri binafsi wakitumia fedha nyingi kununua vipuri vya magari mara kwa mara.

Mwananchi lilifika eneo hilo na katika muda wa saa tano ni daladala tano pekee zilipita katika barabara hiyo zikiwa zimejaa kupita kiasi.

Madereva wa Bajaji waliozungumza na Mwananchi wamesema hawatumii barabara hiyo kutokana na kuwa mbovu.

 “Tunafanya safari za huku lakini hazina faida, hili Toyota DCM tunalitumia lakini kila wiki linakula si chini ya Sh400,000 kwa ajili ya matengenezo,  ukizubaa tu inakula fedha nyingi zaidi, shockup za magari ndizo hasa changamoto,” amesema Hafidh Omary dereva wa daladala.

Mmoja wa wakazi wa Makongo Juu, Emmy Richard amesema ana zaidi ya miezi sita tangu amehamia eneo hilo lakini changamoto kubwa ni usafiri.

Pia Soma

Advertisement
“Ninatumia Bajaji mara nyingi na kama unavyoona milima na haya mabonde na mimi ni mjamzito, hali si nzuri kwa kweli Serikali ilione hili na kutusaidia,” amesema.

Emanuel Rugachwa, dalali maarufu wa eneo hilo akiwa anafanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka 12 amesema barabara hiyo ni tatizo licha ya kutumiwa na wakazi wa Madale, Mbezi, Goba na wengineo.

Rugachwa amesema usafiri wa pikipiki ni changamoto, wajawazito hupata shida.

“Mimi ni dalali watu wengi wanapapenda Makongo Juu ni karibu na mjini, nyumba nzuri lakini wapangaji wanakwambia wazi kuwa mishahara yao itaishia kutengeneza shockup na magari yao,” amesema Rugachwa.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo aliliambia Mwananchi kuwa Serikali inafahamu kuhusu kero ya barabara hiyo na imejipanga kuzitatua.

Chongolo amesema fedha za ujenzi zimeshatengwa kinachosubiriwa ni utaratibu wa fidia kwa awamu ya pili.

Chanzo: mwananchi.co.tz