Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakazi Kurasini walalamikia kubomolewa nyumba zao

Tue, 22 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baadhi ya wakazi wa eneo la Kurasini jijini Dar es Salaam wameilalamikia Manispaa ya Temeke kwa kubomoa nyumba zao na kupuuzia agizo la Mahakama Kuu lililowataka wakae pamoja kujadili mgogoro baina yao na kukubaliana.

Tayari nyumba tatu zimebomolewa alfajiri ya leo Jumapili Januari 20, 2019  na kuzikosesha makazi familia zinazoishi kwenye nyumba hizo.

Nyumba zilizobomolewa ni mali ya Rajabu Msafiri, Athumani Kadukadu na Hashimu Mwambashi.

Akizungumzia suala hilo, mkazi wa eneo hilo ambaye pia nyumba yake iko hatarini kubomolewa, Eliakimu Mwakasisi amesema eneo hilo lilibaki na nyumba 11 lakini baada ya kubomolewa nyumba tatu, sasa zimebaki nane.

Amesema mgogoro huo ulianza mwaka 2013 baada ya Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) kufanya tathmini katika eneo hilo na kutoridhika nalo, hivyo likawa mikononi mwa Manispaa ya Temeke.

“Manispaa walibomoa baadhi ya nyumba kwenye eneo la mradi na kuleta mwekezaji mwingine ambaye ni kampuni ya Cigo.”

“Walilipa fidia na kusema kama kuna mtu hajaridhika na fidia aende mahakamani, basi baadhi ya watu ambao hatukuridhika tulienda mahakamani,” amesema.

“Tulifungua kesi yetu namba 61 mwaka 2017 na mara ya mwisho tulikuwa mahakamani, Jaji akatoa ushauri tukae pamoja na manispaa ya Temeke tujadili suala la fidia, tukikubaliana basi tuandike na kuwasilisha mahakamani, kitu ambacho hakijafanyika mpaka sasa,” amesema.

Mwakasisi amesema leo alfajiri wameshangaa kuona watu wa manispaa wanakuja kuvunja nyumba wakati kesi bado iko mahakamani.

Hata hivyo, amesema mkuu wa upelelezi wa wilaya alisimamisha bomoabomoa hiyo baada ya kubaini kwamba wabomoaji hao waliosindikizwa na mgambo hawakuwa na agizo la Mahakama (court order) na hawakutoa taarifa polisi.

“Tulimsikia mwanasheria wa manispaa akisema lazima tuondoke ili mwekezaji apate eneo lake kwa sababu anawadai na wasipofanya hivyo, Jumatatu atawapeleka mahakamani,” amesema Mwakasisi.

Alipoulizwa kama amepata taarifa za bomoabomoa hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Lusubila Mwakibibi alikana na kujibu kwa kifupi “sijapata”.

Alipoulizwa tena kama anajua kuna kesi Mahakama Kuu kuhusu bomoabomoa katika eneo la Kurasini, Mwakibibi alijibu “ndiyo nasikia kwako”. Baada ya majibu hayo, mkurugenzi huyo akakata simu.



Chanzo: mwananchi.co.tz