Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakazi Kinyerezi wamshatakia RC Chalamila

Kinyerezi Pic Wakazi Kinyerezi wamshatakia RC Chalamila

Fri, 3 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakazi wa Kinyerezi mwisho wamemuomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kuangalia namna ya kuwajengea daraja Mto Kinyerezi ili kuondoa changamoto ya kukatika kwa mawasiliano wakati wa mvua.

Wametoa kauli hiyo ikiwa ni siku ya tatu sasa wakazi wa maeneo hayo wakikiri kuvuka mto huo kwa shida huku wakilazimika kulipia Sh1000 au Sh500 ili waweze kuvushwa kwa kubebwa mgongoni au kwa bodaboda.

Ombi hilo wamelitoa mbele ya RC huyo alipotembelea eneo hilo na kushuhudia shughuli mbalimbali za uvushaji watu zikifanyika kwa pikipiki na kubebwa mgongoni.

"Kutokana na kukosekana kwa daraja katika mto huu, mvua inaponyesha mawasiliano hukatika ambapo wa huku stendi wanabaki huku na wa kule ng'ambo wanabaki hukohuko na hii inafanya baadhi ya shughuli kusimama," amesema Maimuna Msangi, mkazi wa Kinyerezi.

Amesema uwepo wa mvua umekuwa ukiondoa matumaini ya kupata baadhi ya huduma kwa watu wanaoishi ng'ambo ya mto huo kwani wamekuwa wakilazimika kuchagua kubaki nyumbani ili kunusuru maisha yao kutokana na baadhi ya watu kuwahi kubebwa na maji katika eneo hilo.

Rashid Issa ambaye ni mkazi wa Kinyerezi Kanga ambaye anaishi ng'ambo ya mto huo amesema amelazimika kuzuia watoto wake wawili kwenda shule kwa siku ya pili leo kwa kuhofia usalama wao.

"Kwanza kuvuka hapa wawili wawe na 1000 kwenda na Sh1000 kurudi naitoa wapi bado hela ya matumizi, bado hujawapa hela ya matumizi. Kama haitoshi upo kazini huko mvua ikinyesha unawaza watoto wapi katika hali gani tunaomba Serikali itusaidie," amesema Issa.

Issa ametumia nafasi hiyo kuionba Serikali kuwajengea hata kivuko cha watembea kwa miguu ili waweze kuondokana na shida hiyo inayojirudia kila msimu wa mvua.

Rukia Mwaita ambaye ni mwanafunzi anakiri kupata shida ya kuvuka anapofika eneo hilo kwani hulazimika kumsubiri ntu atakayemuonea huruma ili aweze kumpeleka upande wa oili shule ilipo au nyumbani.

Kuna siku unalipa Sh500 siku nyingine hulipi, kama huna unaweza simama hadi nusu saa kama hajapatikana wa kukuonea huruma akuvushe na huwezi kuvuka mwenyewe kwa sababu maji yanapita kwa kasi," amesema Rukia.

“Kuna siku unalipa Sh500 siku nyingine hulipi, kama huna unaweza simama hadi nusu saa kama hajapatikana wa kukuonea huruma akuvushe na huwezi kuvuka mwenyewe kwa sababu maji yanapita kwa kasi," amesema Rukia.

Diwani wa kata ya Kinyerezi Leah Bernard amesema kufuatia suala hilo wamekuwa wakikosa usingizi wakati wa mvua kutokana na simu za wananchi wakilalamikia uwepo wa mto huo.

Hiyo ni kutokana na kile alichoeleza kuwa wakati wa mvua watu wamekuwa wakishindwa kuvuka kufuata huduma za muhimu kama hospitali iliyopo eneo la Kinyerezi.

"Mto huu watu wengi wameshabebwa mbua zinapokuwa kubwa, tunaomba tupate hata kivuko cha waenda kwa miguu, tunaomba tuoate suluhisho la kudumu kuhusu huu mto maana unahatarisha familia zetu,"

Kutokana hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliwataka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) kuakaa kwa pamoja na Timu ya Mkurugenzi wa jiji ili kuangalia nini kinaweza kufanyika.

Hiyo ni kutokana na kuwa eneo hilo linapitisha miundombinu iliyo chini ya TPDC na Tanesco hivyo kabla ya chochote kufanyika ni lazima washirikishwe.

"Tukijithibitishia kuwa tunaweza kufanya kitu, Jumatatu Tarura muwe hapa asubuhi kuangalia namna ya kuweka kivuko kisichokuwa na gharama kubwa mimi niko tayari kuifhinisha fedha kwa mkurugenzi wa jiji ili kushughulikia suala hili,"

Aliwataka Tarura kuweka mchoro ambao si wa gharama kubwa ili usije kukwamisha kusaidia wananchi huku akieleza kuwa kama eneo hilo halitakuwa na barabara iangaliwe sehemu barabara ilipo ili ijengwe.

"Hii ikiwa na maana kuwa wale ambao watakuwa wamejenga kwenye eneo la barabara hiyo itatakiwa kupita wajiandae kupisha siku hizi chache ili tuweke barabara hata kama umejenga ghorofa," amesema Chalamila.

Aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhali juu ya uwepo wa mvua hizi ambazo zimetangazwa kuwa zitakuwapo kwa miezi mitatu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live